Home KITAIFA Dc Dodoma atoa wito ushirikiano katika elimu ya usalama barabarani

Dc Dodoma atoa wito ushirikiano katika elimu ya usalama barabarani

Na Amani Nsello- Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri ametembelea banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika Maonesho ya wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma, ambapo ametoa wito kwa taasisi hiyo kushirikiana na taasisi nyingine na vyama vya waendesha bodaboda katika kutoa elimu ya usalama barabarani ili kusaidia kupunguza ajali.

Akizungumza katika banda hilo, leo Agosti 6, 2025 Shekimweri ameipongeza MOI kwa kazi kubwa ya kutoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa wahanga wa ajali, na kutoa wito kwa taasisi hiyo kusaidia jamii kupitia elimu na uhamasishaji wa kupunguza ajali hizo.

“Nawapongeza MOI kwa kazi nzuri mnayofanya, lakini nawasihi mshirikiane na taasisi kama VETA na vyama vya bodaboda kama UWAMIDO ili kuwafikia waendesha bodaboda wengi zaidi kwa elimu ya usalama barabarani… Hii itasaidia kupunguza ajali na ulemavu unaotokana na uzembe au kutozingatia sheria,” amesema Shekimweri

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa ushauri kufanyika kwa ziara maalum za waendesha bodaboda kutembelea majeruhi waliolazwa MOI kutokana na ajali za barabarani ili kujifunza kwa vitendo athari za ajali na kuchukua tahadhari.

Kwa upande wake, Daktari bingwa wa Radiolojia wa MOI, Dk. Angela Isangya amemwambia Mkuu huyo wa Wilaya kuwa taasisi iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za kuzuia ajali hususani kwa kutoa elimu ya kinga na usalama barabarani.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025” yalianza Agosti 1 na yatafikia tamati Agosti 08, 2025 katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here