Home KITAIFA Machali ahamasisha wananchi kujitokeza kupata ujuzi VETA

Machali ahamasisha wananchi kujitokeza kupata ujuzi VETA

Na Esther Mnyika,Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata mafunzo ya ujuzi yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa.

Akizungumza Agosti 6,2025 wakati alipotembelea Banda la VETA lililopo kwenye Maonesho ya Wakulima na wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Machali amesema ameshuhudia mafanikio ya moja kwa moja kwa vijana na wanawake waliopata mafunzo ya ufundi na ujasiriamali kupitia VETA.

Amesema kuwa mafunzo yanayotolewa na VETA ni ya vitendo na hujikita katika kumpa mtu ujuzi wa moja kwa moja unaoweza kumpatia kipato, hivyo kuwataka wananchi kutokupuuza fursa hiyo muhimu.

“Nimepita hapa VETA naona kabisa kuna watu waliowezeshwa. Wanawake na vijana wamejifunza kuchakata bidhaa za kilimo na kuziongezea thamani. Wapo wanaotengeneza sabuni, juisi, biskuti, na bidhaa nyingine nyingi,” amesema.

Ameongeza kuwa mafunzo yanayotolewa na VETA ni ya vitendo na hujikita katika kumpa mtu ujuzi wa moja kwa moja unaoweza kumpatia kipato, hivyo kuwataka wananchi kutokupuuza fursa hiyo muhimu.

“Wito wangu kwa wananchi, hata sisi wakubwa, twendeni VETA. Si kwa ajili ya cheti tu, bali kwa ajili ya kujifunza ujuzi wa maisha. VETA wanakupa ujuzi wa moja kwa moja, unajifunza kutengeneza bidhaa, kuchakata vyakula, hata ufundi stadi mbalimbali,” amesisitiza Machali.

Aidha, amewapongeza viongozi na wakufunzi wa VETA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwainua wananchi kupitia elimu ya ufundi, huku akizitaka halmashauri na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kufikia watu wengi zaidi.

Maonesho ya Nanenane yamekuwa jukwaa muhimu kwa VETA kuonesha kwa vitendo mafanikio ya elimu ya ufundi, na mwaka huu yameendelea kuonesha jinsi elimu hiyo inavyoweza kubadili maisha ya wananchi kwa kutoa suluhisho la ajira na kuongeza tija katika sekta ya kilimo na viwanda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here