Na Esther Mnyika, Dodoma
WAKULIMA na Wafugaji nchini wametakiwa kuchangamkia fursa ya bima za kilimo na mifugo ili kulinda uwekezaji wao dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri uzalishaji wao.

Akizungumza Agosti, 8 2025 Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk. Baghayo Saqware wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane ambayo kitaifa yaliyofanyika jijini Dodoma.
Amesema kushiriki maonesho hayo ni kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wa misitu kuhusu umuhimu wa bima, hususan katika kipindi ambacho serikali imewekeza zaidi kwenye Mpango wa Kilimo wa BBT (Building a Better Tomorrow).
“Tumejipanga kutembelea kila mkoa kuongea na wakulima ili waelewe namna ya kujiunga na mfumo wa bima za kilimo na afya. Tunawaomba wakulima watembelee kampuni 15 zinazotoa huduma hizi,” amesema Dk. Saqware.
Amebainisha kuwa mwaka 2023, kampuni za bima zililipa zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa wakulima wa tumbaku mkoani Tabora waliopata hasara kutokana na majanga, fedha zilizotokana na mfuko wa pamoja wa kampuni za bima za kilimo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance na mwakilishi Kosantia la Bima za Kilimo (TAIC), Wilson Mzava amesema umoja huo umeundwa ili kuhakikisha bima bora za kilimo zinapatikana kwa bei nafuu, na malipo ya fidia yanafanyika haraka pindi majanga yanapotokea.
“Nguvu ya umoja huu inatufanya tufikie wakulima wengi zaidi na kupunguza hasara kwa kampuni moja pale majanga yanapotokea,” amesema Mzava.
Kwa upande wake Msajili Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania (TIO), Jamali Mwasha, amesema ofisi yake ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima Namba 10 ya mwaka 2009 na Kanuni Namba 6 ya mwaka 2013, kwa lengo la kutatua migogoro ya bima kwa njia mbadala ili kulinda maslahi ya mtoa huduma na mteja na kukuza imani ya wananchi katika sekta ya bima.
Amesema majukumu ya TIO ni pamoja na kusajili migogoro stahiki, kutoa ushauri kwa walalamikaji na makampuni ya bima, kufanya usuluhishi, upatanishi na kutoa maamuzi.
“Tupo hapa Nanenane kutoa elimu ili wananchi wajue kuna ofisi rasmi ya kushughulikia migogoro ya bima. Wanapokumbana na changamoto katika madai yao, wasikate tamaa bali wawasilishe malalamiko yao kwetu ili tuyashughulikie kwa mujibu wa sheria,” amesema Mwasha.
Ameeleza kuwa, migogoro hiyo inaweza kuhusisha madai yaliyokataliwa, kama vile fidia ya nyumba iliyoungua, gari lililopata ajali au hasara nyingine zilizokatiwa bima.