Home KITAIFA Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mto Malagarasi, wapiga hatua mpya

Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mto Malagarasi, wapiga hatua mpya

📌Mto wachepushwa ili kujenga tuta la kufulia Umeme

📌Kasi yapamba moto kukamilisha Mradi

Na Mwandishi wetu,

UJENZI wa Mradi wa Bwawa la kufua umeme kwa maji kupitia mto Malagarasi (MW49) umefikia hatua muhimu, kwa kuweza kuchepusha maji ya kwenye mto (kutengeneza njia ya maji) ili kuruhusu ujenzi wa Tuta kuu,litakalotumika katika kufua umeme.

Akizungumza katika hafla fupi ya uchepushaji maji, Agosti 13,2025 Meneja wa Mradi Mhandisi Saidi Kimbanga amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika utekelezaji wa mradi huo ambao kwa sasa ujenzi wa mradi umefikia kwa Asilimia 10, na unatarajia kukamilika mwanzoni kwa mwaka 2027.

“Ujenzi wa mradi unaenda kwa kasi sana, uchepushaji maji ulitakiwa kufanyika tarehe 27, mwezi huu, lakini tumefanikisha zoezi hili leo, siku zaidi ya kumi nyuma, hivyo tunatarajia hata mradi utakamilika mapema zaidi” amesema Mhandisi Saidi.

Akizungumzia umuhimu wa uchepushaji maji, Mha. Saidi amesema kuwa maana nzima ya ujenzi wa Bwawa la kufua umeme unahitaji kuweza kudhibiti maji ili yaweze kupita katika njia maalum, na kuweza kufua umeme, hivyo hatua hii ni muhimu ilikuweza kuzalisha umeme uliokusudiwa kupatikana.

Naye Mkurugenzi wa Kanda ya Magharibi Mhandisi Andrew Swai akizungumza amesema kuwa hatua hiyo muhimu imetokana na Mchango mkubwa wa Serikali, Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kuweza kuhakikisha na kumsimamia Mkandarasi (Dongfang Electric International Corporation kutoka China) ili kukamilisha kazi hiyo na ameahidi kuwa Mradi wa Malagarasi utakamilika na TANESCO haitalala, itashirikiana na Mkandarasi katika kuhakikisha mradi una kamilika kwa wakati.

Kwa upande mwingine, Meneja wa Mkoa wa Kigoma Mhandisi Julius Sabu, amesema kuwa Kukamilika kwa Mradi wa Malagarasi kutaongeza umeme hata katika Mkoa wa Kigoma na kusema kuwa Kigoma sasa itakua na umeme wa uhakika, na kuwataka wawekezaji kuanza kuwekeza katika Mkoa wa Kigoma.

Ujenzi wa Mradi wa Malagarasi wa Megawati 49.5 unatekeleza na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania, ambapo ulianza Aprili 10,2024 na unatarajia kukamilika Oktoba 10,2027, gharama za Mradi za ujenzi wa Bwawa ikiwa ni Shilingi Bilioni 300 za Kitanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here