Home KITAIFA Dk.Biteko azindua programu ya uatoaji wa majiko ya umeme kwa bei ya...

Dk.Biteko azindua programu ya uatoaji wa majiko ya umeme kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi wa TANESCO

📌 Takribani Majiko 11,000 kutolewa kwa wafanyakazi kwa bei ya ruzuku kupitia mfuko wa mzunguko

📌 Asisitiza programu hiyo ya TANESCO ni uthibitisho wa jitihada za utekelezaji wa maono ya Rais Samia kwa vitendo

Na Mwandishi wetu, Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko , leo Agosti 14, 2025, amezindua Programu ya Utoaji wa Majiko ya Umeme kwa Bei ya Ruzuku kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Hatua hii inalenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa nishati zisizo salama.

Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete, Dodoma, na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, Bodi na Menejimenti ya TANESCO pamoja na wadau wa sekta ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dk. Biteko amesema kuwa mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034, unaolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya kaya nchini zinatumia nishati safi, salama na nafuu ya kupikia.

Amepongeza Rais wDk. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi na maono yake ya kuhakikisha Watanzania wanapata nishati salama na rafiki kwa mazingira, akibainisha kuwa mpango huu wa TANESCO ni ushahidi wa utekelezaji wa maono hayo.

“Napenda kuwapongeza TANESCO kwa mpango huu, ambao unathibitisha jitihada zao za dhati katika utekelezaji wa maono ya Rais Samia kwa vitendo. Utaratibu wa malipo kwa awamu ni ubunifu unaowawezesha wafanyakazi kujiunga na mpango bila kubeba mzigo mkubwa wa kifedha kwa wakati mmoja,” amesema Dk. Biteko.

Amefafanua kuwa programu hii inatekelezwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Modern Energy Cooking Services (MECS) chini ya Serikali ya Uingereza. Kupitia mpango huu, TANESCO imenunua majiko janja 11,000 yatakayotolewa kwa wafanyakazi kwa bei ya ruzuku kupitia mfuko wa mzunguko (Revolving Fund).

Aidha, wafanyakazi watanufaika kwa kupata majiko hayo kupitia njia rahisi za malipo ikiwemo malipo ya moja kwa moja na malipo kwa awamu kupitia makato ya mishahara.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Balozi Zuhura Bundala, akimuwakilisha Mwenyekiti wa Bodi hiyo, amesema kuwa tukio hili linaweka alama muhimu katika safari ya kuibadilisha Tanzania kuwa Taifa linalotumia nishati safi, salama na endelevu, ambapo TANESCO imetimiza kwa vitendo kwa kuhamasisha wafanyakazi wake kuwa mabalozi wa mabadiliko hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema kuwa uzinduzi huu wa mpango wa kutoa majiko kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi wa TANESCO ni fursa ya kipekee ya kuwapa motisha kuwa mstari wa mbele katika kutumia nishati safi na kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii, huku akiweka mkazo kwamba ajenda inaanza na wafanyakazi ili Watanzania wote wafuate mfano huo.

Mpango huu unatarajiwa kuboresha afya na ustawi wa wananchi, kulinda mazingira, kuongeza mapato ya Shirika kupitia wateja wanaopikia kwa umeme, na kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata nishati salama na nafuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here