Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
MSAJILI wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi amewaasa wagombea wa vyama vya siasa katika kuelekea kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kutotumia lugha za matusi ambazo msingi wake ni kuchochea kuvuruga amani ya nchi.

Pia amesema kampeni za kistaarabu zinasaidia kuleta utulivu katika kipindi chote cha kampeni hadi uchaguzi mkuu.
Hayo ameyabainisha leo Agosti, 18 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa, Jaji Mutungi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uelewa wa kutekeleza sheria katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mkuu.
Amesema lengo la hayo ni kuongeza uelewa wa kutekeleza sheria hiyo na ni muhimu kwao na kuwa mabalozi wazuri kwa wengine.
“Naomba niseme kuwa kuna maisha baada ya chaguzi hivyo amani ya taifa ipewe kipaumbele chake katika uchaguzi huu nchi ikingia kwenye machafuko hakutakuwawa na siasa wala amani hivyo tuwe mabalozi wazuri wa kutunza amani ya nchi,”amesema.

Amesema waendelee kurithisha amani iliyo tengenezwa na waasisi wetu kwa vizazi vijavyo.
Jaji Mutungi amewasisitiza wagombea watakapokuwa wanafanya kampeni zao watangeze sera za vyama vyao kwa wananchi na kufanya kampeniza kistaarbu.
Ameongeza kuwa viongozi lazima wawe mfano mzuri kwa watanzania inapofika kipindi cha uchaguzi kunakuwa na mambo mengi hasa katika mitandao ya kijamii hivyo wanatakiwa kuwa makini.
“Viongozi tunatakiwa kuwa na msimamo unaweza ukaamka asubuhi ukaona taarifa za uvumi zinasema hakuna uchaguzi hivyo tupuuze mambo hayo uchaguzi upo na utafanyika tunafanya Uchaguzi wa amani na haki,”amesema.

SHERIA YA UKOMO WA GHARAMA
Akizungumzia sheria ya ukomo wa gharama za uchaguzi sura ya 278 iliyotungwa mwaka 2010 nakufanyiwa marekebisho mara kadhaa imeweka shariti la kuweka wazi mapato na matumizi gharama za uchaguzi.Ili kuhakikisha fedha zitakazotumika zinatokana na vyanzo halali vya kisheria kuhakikisha matumizi yote ya gharama za uchaguzi kufanyika kwa mujibu wa sheria.
Pia sheria hiyo inaweka ukomo wa gharama za matumizi kwa kila nafasi anayogombea .
Hata hivyo baadhi ya washiriki walitoa maoni yao katika kikao hicho walidai utekelezaji wa sheria hiyo itakuwa ni mgumu kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu amewataka viongozi na watendaji wa vyama vya siasa nchini kuzingatia kwa makini masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuepusha dosari na kasoro katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Pia amempongeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi, kwa hatua ya kuwaleta pamoja viongozi wa kitaifa na watendaji wa vyama kwa lengo la kutoa elimu na kuimarisha msingi wa demokrasia.
“Mgeni Rasmi, tunakupongeza sana kwa kazi nzuri ya ulezi wa vyama vya siasa. Umeona umuhimu wa kutukutanisha hapa ili kupitia Sheria ya Gharama za Uchaguzi, jambo hili ni jema kwa sababu linapunguza kasoro katika uchaguzi wetu,” amesema Khatibu.
Amesisitiza kuwa historia inaonesha baadhi ya vyama na wagombea walikuwa na uelewa mdogo walipotakiwa kuwasilisha taarifa za gharama za uchaguzi, jambo lililosababisha kuibuka kwa kasoro kubwa.
“Sheria hii ilipokuja mwaka 2010, watu wengi hawakuwa na uelewa. Wengine walijaza gharama za uchaguzi hewa wakidhani baada ya uchaguzi wangerejeshewa fedha. Watu walitengeneza risiti za kughushi, kumbe haipo hivyo. Hivyo basi leo tunatarajia kupata elimu ya kutosha,” amefafanua.
Khatibu amewataka viongozi na watendaji wa vyama kuchukua kwa umakini mkubwa mafunzo hayo ili, kuelekea Uchaguzi Mkuu, zoezi la kampeni na uchaguzi kwa ujumla liendeshwe kwa uwazi, uadilifu na kuepusha migogoro.