Na Mwandishi Wetu – Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na taasisi za dini kuimairisha ushirikiano na Serikali na kujiunga katika mtandao wa kitaifa wa usimamizi wa huduma za kibinadamu.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi wakati akimwakilisha Waziri Mkuu katika Maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Misaada ya Kibinadamu Duniani Agosti, 19 2025 Jijini Dodoma.
“Ninatoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na taasisi za dini kuimairisha ushirikiano na Serikali na kujiunga katika mtandao wa kitaifa wa usimamizi wa huduma za kibinadamu, kwa kufanya hivyo kutaongeza uratibu, uwajibikaji na ufanisi katika kushughulikia majanga,” ameeleza.
Aidha, amesisitiza watoa huduma za kibinadamu kutia mkazo katika suala la kuelimisha umma ili wananchi waweze kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu ili kuweza kupunguza athari za majanga pindi yanapotokea.

“Kwa kuwa yapo majanga ambayo hayakwepeki, ninawasihi sana watoa huduma za kibinadamu, kutilia mkazo suala la kuelimisha umma. Wananchi waelimishwe kuzingatia maelekezo yanayotolewa na watalaamu ili kupunguza athari za majanga yanapotokea,”amefafanua.
Mbali na hayo amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mikakati na kampeni zote za uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha katika kukabiliana na majanga hususan yale ya asilia.
“Suala na utunzaji wa mazingira ni muhimu sana katika kukabiliana na majanga hususan yale ya asilia, nitoe wito kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mikakati na kampeni zote za uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Hatua mojawapo muhimu ni kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi hivyo niwakumbushe Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika kampeni hizo muhimu za Kitaifa,”amesisitiza.
Akizungumza kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge unaotarajiwa kufanyika 29 Oktoba, 2025 amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika kuwachagua Viongozi wao akiwemo Rais, Wabunge na Madiwani.

“Tujitokeze kwa wingi kutumia haki yetu ya kikatiba, kila Mtanzania atambue kuwa kupiga kura ni haki na wajibu wake ili kuwapata viongozi bora watakaoharakisha maendeleo ya taifa letu,” amesisitiza Waziri Lukuvi.
Maadhimisho ya Siku ya Watoa Misaada ya Kibinadamu Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 19 Agosti, Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 inasema“Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Kibinadamu na Ustahimilivu Dhidi ya Majanga.”