Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema elimu ya watu wazima sio tu elimu ya masomo ya kawaida, bali ni zana muhimu ya maendeleo endelevu, kwani inachangia kipato, ustawi wa kijamii, afya na ushiriki wa kiraia.

ameongeza kuwa uzoefu duniani unaonesha kwamba elimu ya watu wazima ni chombo muhimu cha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na binafsi.
Amesema hayo leo Agosti 25, 2025 alipofungua kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Elimu si tukio la muda bali ni safari endelevu ya kujifunza katika maisha yote, elimu ya Watu wazima si kwa ajili ya watu wazima pekee, bali hata kundi la vijana wanaweza kujiunga na kunufaika na program mbalimbali za ujuzi zinazotolewa na taasisi hiyo,”amesema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua kwamba katika kipindi cha nusu karne iliyopita, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imepiga hatua kubwa na kutoa mchango wa kipekee katika maendeleo ya Taifa.

“Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imekuwa ikishauri Serikali kwenye maeneo ya kisera na kitaalamu katika masuala ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi iliyosaidia kuwafikia Watanzania wengi zaidi waliokuwa hawajapata fursa ya elimu ya msingi;”amesema.
Majaliwa ameielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuhakikisha wanaongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya watu wazima ikiwemo kuwafikia makundi yote nchini hasa maeneo yaliyo pembezoni na yenye changamoto za kijamii na kijiografia.
Pia, ameiagiza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa kushirikiana na wadau waendelee kufanya tafiti za mara kwa mara kuhusiana na elimu ya watu wazima ili kubaini changamoto zinazojitokeza na kuandaa suluhisho bunifu linaloendana na mahitaji halisi ya jamii.

Naye, Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati ikiwemo mradi wa SEQUIP (Secondary Education Quality Improvement Project) ambapo umefanikiwa kuwarejesha wasichana 13,272 katika mfumo wa elimu katika kipindi cha miaka mitano.
Amesema kuwa mradi mwingine ni IPOSA (Integrated Programme for Out-of School Adolescents) ambao umewezesha kuwajengea uwezo vijana 10,000 walioko nje ya mfumo rasmi katika maeneo ya stadi za maisha, ujasiriamali na ufundi wa awali
Kwa Upande wake Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Profesa Philipo Sanga amesema kuwa Taasisi hiyo inajivunia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita hasa katika kuboresha mifumo ya elimu ikiwemo sera ya elimu jumuishi ambayo inagusa makundi yote pasipo ubaguzi.