Home SIASA Flatei atimka ACT arejea CCM kusaka kura za ushindi

Flatei atimka ACT arejea CCM kusaka kura za ushindi

Na Mwandishi wetu, Manyara

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Mbulu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Flatei Maasai ametangaza kurejea CCM akitokea ACT Wazalendo ambako aliteuliwa kugombea ubunge kupitia chama hicho huku akisisitiza kumuombea kura mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza wilayani Mbulu akiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, Flatei alisema baada ya kuhama CCM alikutana na wazee ambao walimlea tangu akiwa mdogo wakimtaka kurejea ndani ya Chama.

“Nilikutana na wazee wangu wa Chama ambao walinilea tangu nilipokuwa mtoto hadi leo, basi nikaona nikubali kurejea Chama Cha Mapinduzi. Kwa sisi watu wa Mbulu wakishakuja wazee wakikwambia kijana acha hivi na sisi tunaita wazee wa jani, likiwekwa jani la kijani mbele yao huwezi kuendelea tena.

“Inabidi uwasikilize wazee wanasema nini, na mimi ninavyojua wazee hao ni wazee wangu na kwa sababu hawa wazee ni wa Chama wamekuja kwangu, zaidi ni kuwasikiliza wazee hawa ili kuendelea kujenga Chama,” ameeleza.

Kwa upande wake, Wasira, ametoa wito kwa wanachama wa CCM ambao hawajateuliwa kugombea ubunge, kuendelea kumuombea kura mgombea Urais wa CCM Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa chama hicho.

Amesema kutoteuliwa kugombea nafasi hiyo siyo mwisho wa uanachama wa CCM kwani chama hicho kingeshakuwa kimepoteza idadi kubwa ya wanachama ambao hawajateuliwa kuwania nafasi hiyo kupitia CC.

Wasira alisema alipofika Mbulu alizungumza naye na kumshauri kwamba uanachama wake ndani ya CCM siyo lazima mpaka awe mbunge.

“Mbona wapo wengine wanachama lakini siyo wabunge, lakini kazi za kujenga chama na kujenga nchi siyo Bunge peke yake, zipo nyingi hata kusimama kwenye jukwaa na kuwaambia chagua Samia. Hiyo ni kazi ya CCM ambayo huyu anaiweza na tumemwambia aende jukwaani akaombe kura,” amesisitiza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here