Home UCHUMI Mziray: Benki ya NCBA imelenga kusaidia jamii

Mziray: Benki ya NCBA imelenga kusaidia jamii

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya NCBA, Alex Mziray, amesema benki hiyo imelenga kuisaidia jamii kuwa na uamuzi wa kifedha ili kuleta mabadiliko katika nchi na jamii kwa ujumla.

Mziray amesema hayo leo Septemba3,2025 wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni ya kimkakati ya Maisha ni Hesabu ambayo inalenga kuonyesha namna inavyoweza kuleta mabadiliko.

Amesema kampeni hiyo siyo tu kauli mbiu ya kimasoko, bali ni tamko la dhamira ya benki kushiriki moja kwa moja katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

“Kupitia kampeni hii, tunataka kuonesha kuwa kila shilingi inayowekezwa, kila mkopo unaotolewa na kila huduma tunayotoa, ni namba yenye maana ,namba inayogusa maisha ya mtu, biashara au jamii kwa ujumla,” amesema Mziray.

Mziray amebainisha kuwa NCBA imeendelea kuwekeza katika sekta kuu za uchumi zikiwemo viwanda, mawasiliano, mafuta na gesi, pamoja na sekta ya usafirishaji. Kupitia huduma za kifedha, benki imesaidia wateja wake kupanua biashara, kuongeza mapato na kuimarisha nafasi zao sokoni.

Aidha, amesema kuwa NCBA inaona wajibu wa kuhakikisha ukuaji wa kiuchumi unakwenda sambamba na hifadhi ya mazingira.

Akizungumzia mipango ya mazingira, Mziray amesema NCBA imepanga kupanda miti zaidi ya 10,000 ifikapo mwisho wa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya kujali jamii na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tayari tumeanza Zanzibar, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam. Kwa mfano, hivi karibuni tulipanda miti 5,000 kando ya Mto Mpiji Bunju B ili kupunguza mmomonyoko wa ardhi na kulinda vyanzo vya maji,” amesema.

Mziray amesisitiza kuwa NCBA itaendelea kutoa suluhu bunifu kwa wateja wake, ikiwemo NCBA ‘Now App’ inayowezesha huduma za kibenki kidigitali.

Amefafanua kuwa kutokana na mageuzi hayo, benki imefanikiwa kuongeza faida kabla ya kulipa kodi kwa asilimia 24 kutoka Sh bilioni 13.0 mwaka 2023 hadi bilioni 16.1 mwaka 2024.

Mbali na huduma za kifedha, Mziray aligusia mchango wa NCBA Golf Series, akisema mashindano hayo yamekuwa chachu ya kukuza vipaji vipya vya vijana na wanawake huku yakiimarisha mshikamano wa kijamii na kutoa fursa za mtandao wa kibiashara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here