Na Florah Amon, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano kubwa la kimataifa la wafugaji wa nguruwe Barani Afrika litakalofanyika Septemba 11 hadi 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 3 2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Nguruwe Tanzania (Tanzania Association of Pig Farmers ( TAPIFA), Doreen Maro, amesema kongamano hilo la kihistoria linalenga kujadili mnyororo wa thamani wa ufugaji wa nguruwe na sekta nzima kwa ujumla.
“Ni kongamano ambalo halijawahi kufanyika nchini kwetu, ni mara ya kwanza, na litawaleta pamoja wadau kutoka nchi mbalimbali za Afrika,” amesema Doreen.
Ameeleza kuwa kongamano hilo linatarajiwa pia kushirikisha wadau wa sekta hiyo pamoja na wataalamu ambao watawasilisha tafiti na kutoa elimu kwa wafugaji.
Doreen amesema zaidi ya vyama tisa kutoka barani Afrika vimeshathibitisha kushiriki, huku akihimiza wadau wenye nia ya kushiriki kujisajili mapema.
Ameongeza kuwa moja ya malengo makuu ya kongamano hilo ni kuwajengea uwezo wafugaji wadogo na wa kati ili waweze kuendesha shughuli zao kibiashara na kushindana kwenye soko la ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia hali ya ulaji wa nyama ya nguruwe, Doreen amesema kuwa kiwango chake kimeongezeka, ambapo pia aliitaka Serikali kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji, hususan changamoto za machinjio.
Kwa upande wake, Mdhamini Mkuu wa kongamano hilo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kupitia Meneja Masoko wake, Richard Steven, amewataka wafugaji wa nguruwe kujitokeza kwa wingi ili wapate elimu ya fedha na mikopo kupitia benki hiyo.
Steven amebainisha kuwa TADB imejipanga kutoa mikopo yenye masharti nafuu itakayowawezesha wafugaji kuboresha miundombinu ya ufugaji, ikiwemo mabanda, huduma za afya ya mifugo na masoko ya uhakika.
Aidha, kongamano hilo linatarajiwa kutoa fursa ya maonesho ya bidhaa na teknolojia mpya za ufugaji wa nguruwe ambapo makampuni mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yatashiriki kuonesha ubunifu na huduma zinazohusiana na sekta hiyo.