Na Mwandishi wetu, Tanga
MGOMBEA urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, akiwa kwenye uzinduzi wa kampeni leo Septemba, 4 2025 jijini Tanga ameeleza dira yake ya uongozi inayotokana na ilani ya uchaguzi ya chama hicho, iliyoegemea kwenye misingi ya Uzalendo, Haki na Maendeleo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Doyo amesema dhamira yake ya kugombea urais imetokana na utashi wake binafsi na imani kwamba ana uwezo wa kuwa kiongozi wa juu wa maamuzi kwa manufaa ya Taifa. Alisisitiza kuwa serikali yake itaongozwa na misingi hiyo mitatu ikiwa kama dira ya msingi mikuu ya uongozi wake.
“Tumechunguza ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kipindi cha miaka sita mfululizo, na hakuna hata moja iliyowafurahisha Watanzania. Baadhi ya wananchi wamekosa uzalendo, wamekuwa wakifuja mali za umma bila kuwajibishwa. Hii inaashiria changamoto kubwa ya uzalendo. Serikali yangu itahakikisha somo mahsusi la Uzalendo linafundishwa kuanzia shule ya msingi,” amrsema Doyo.
Akizungumzia kuhusu sekta ya kilimo, Doyo amesema zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo, lakini bajeti ya sekta hiyo imeendelea kubaki chini ya asilimia 10. Ameahidi kuwa serikali ya NLD itatoa mbegu bora bure, itatafuta masoko, na itaboresha barabara ili wakulima waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuepuka ulanguzi wa madalali. Aidha, alisema katika mikoa ya Pwani kutakuwa na uwekezaji mkubwa kwenye vituo vya kuchakata samaki na ununuzi wa meli tatu kubwa za kuvua samaki Bahari ya Hindi. Hatua hiyo, amesema, itasaidia kuongeza fedha za kigeni na kupunguza ukosefu wa ajira hususan katika ukanda wa Pwani ikiwemo Tanga.

Kwa upande wa huduma za kijamii, Doyo ameahidi kuboresha mfumo wa bima ya afya ili kuhakikisha kila Mtanzania anatibiwa kikamilifu bila vikwazo vya kifedha. Pia alisema serikali yake itaandaa vijana kielimu ili waweze kujiajiri mara tu wanapohitimu masomo yao ya juu.
Kuhusu teknolojia, amebainisha kuwa NLD itajenga vituo vya elimu ya teknolojia katika kila halmashauri. Vituo hivyo vitawawezesha vijana kujifunza, kufanya utafiti na kutoa ushauri kwa serikali. “Dunia imekuwa kijiji. Ni wajibu wetu kuweka teknolojia kama mpango mkakati wa kiuchumi,” aliongeza.
Katika eneo la mahusiano ya kimataifa, Doyo amesema Tanzania haina uhasama na nchi yoyote, hivyo serikali yake itaendeleza mazuri yaliyopatikana, huku ikiunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

“Tunatoa wito kwa Watanzania wote kudumisha amani, mshikamano na umoja. Hapo ndipo inapokuja dira ya uzalendo, haki na maendeleo kama tunu ya Taifa. Tuwe wazalendo wa kweli kwa nchi yetu. Bila amani, hakuna maendeleo, hakuna mshikamano, na hakuna haki. Amani yetu ndiyo msingi wa kila mafanikio ya Taifa,” amesisitiza Doyo.
Chama cha NLD kinatarajia kuendelea na kampeni zake za kumnadi mgombea urais wake katika wilaya za Pangani, Mkinga, Muheza, Lushoto, Korogwe, Handeni, na hatimaye kuelekea Mkoa wa Manyara.