📍Ni katika operesheni maalum ya ukaguzi inayofanywa na TANESCO Nchi nzima
📍TANESCO yasisitiza zoezi ni endelevu na kutangaza kiama kwa waolihujumu Shirika
Na Mwandishi wetu, Morogoro
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewakamata wateja wakubwa wawili mkoani Morogoro ambao ni PH Hotel na Igombe Hotel wakijihusisha na wizi wa umeme ambapo waligundulika kuchepusha nyaya kwenye mita zao aina ya T2 na hivyo kutumia umeme bila kulipa gharama yoyote jambo linalolikosesha Shirika mapato.

Wateja hao wamekamatwa wiki hii ikiwa ni kati ya wateja 14 waliokamatwa katika operesheni hiyo inayohusisha wataalamu wa mita kutoka Makao Makuu TANESCO wakishirikiana na ofisi ya Mkoa wa TANESCO Morogoro Kaskazini.

Timu hiyo ya ukaguzi ilifika katika maeneo ya Msamvu, Morogoro, ambako hoteli hizo zipo, na kufanikisha kubaini hujuma hizo kwa ushirikiano wa viongozi wa Serikali za Mtaa wa White House pamoja na Jeshi la Polisi.


Aidha, Shirika linaendelea kuimarisha ukaguzi na kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo vinavyolikosesha Shirika mapato.