Home SIASA Doyo Aendelea na Kampeni Muheza, Aahidi Kutatua Changamoto za Wananchi

Doyo Aendelea na Kampeni Muheza, Aahidi Kutatua Changamoto za Wananchi

Na Mwandishi wetu, Tanga

MGOMBEA Urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake kwa mfumo wa kijiji kwa kijiji na kata kwa kata. Leo hii alikuwa katika Wilaya ya Muheza, Kata ya Majengo, ambako amewataka wananchi wa eneo hilo kumpa kura ili aweze kutatua changamoto zinazowakabili.

Akihutubia wananchi, Doyo amesema kuwa wakazi wa Muheza wamesahaulika kwa muda mrefu na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), licha ya kuwa eneo hilo lina mchango mkubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga.

“Haiwezekani maji yanayotumika Tanga Mjini yanatoka Muheza, lakini Muheza wenyewe wanateseka na shida ya maji. Yote haya ni kwa sababu mnachagua CCM. Na CCM wenyewe wakidhani hakuna changamoto wala matatizo ya kiuchumi Kwa sababa mnaonyesha kuipenda,” amesema Doyo.

Aidha, ametolea mfano Barabara ya Amani ambayo alisema ni kitovu cha uchumi wa wananchi wa Muheza. Kwa mujibu wake, barabara hiyo imeendelea kutelekezwa kwa ahadi zisizotekelezwa kwa miaka mingi, licha ya kuwa bidhaa muhimu za viungo kutoka Muheza huuzwa hadi kwa fedha za kigeni. “Mkichagua NLD chini ya uongozi wangu, tutahakikisha barabara hii inakarabatiwa mara moja,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkomwa, mmoja wa viongozi wa chama hicho, alisema wananchi wa Muheza wana sababu nyingi za kumuunga mkono Mhe. Doyo, ikiwemo changamoto za miundombinu duni pamoja na maisha magumu yanayowakumba vijana na kina mama.

Naye Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Pogora Ibrahim Pogora, aliwataka wananchi wa Muheza kutofanya makosa ifikapo Oktoba 29, akisisitiza kuwa hali duni ya maisha ya Watanzania imesababishwa na utawala wa CCM.

“Hakuna namna CCM inaweza kujitenga na maisha haya duni ya Watanzania. Sasa muda umefika wa kuwaondoa madarakani,” amesema Pogora.

Kampeni za Chama cha NLD zilianza rasmi Septemba 4 mkoani Tanga na zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini. Baada ya mkutano wa Muheza, msafara wa mgombea urais huyo unatarajiwa kuelekea Korogwe, Lushoto na Handeni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here