Home KITAIFA TBS yaanza utekelezaji wa kanuni ya uongezaji virutubishi kwenye vyakula ya mwaka...

TBS yaanza utekelezaji wa kanuni ya uongezaji virutubishi kwenye vyakula ya mwaka 2024

Na Florah Amon,Dar es Salaam

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeanza utekelezaji kwa kanuni mpya za mwaka 2024 zinazolenga kuongeza virutubisho katika vyakula vinavyotumiwa kwa wingi nchini.

Hayo ameyasema leo Septemba, 8 2025 na Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango wa TBS, David Ndibalema, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wadau husika kwa maana wazalishaji wauzaji na wasambazaji kampeni maalum ya kuelimisha wadau wa sekta hiyo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye bidhaa za msingi kama unga wa mahindi, unga wa ngano, mafuta yaliyosafishwa na chumvi ni za lazima, na utekelezaji wake unalenga kupambana na changamoto ya lishe duni nchini.

“TBS inawataka wasambazaji na wauzaji wote wa unga wa mahindi kuhakikisha bidhaa zao zinaongezwa virutubishi stahiki kabla ya kuingizwa sokon hli si ombi tena, ni hitaji la kisheria kwa ajili ya kulinda afya ya jamii,” amesema Ndibalema.

Ameongeza kuwa uelewa mdogo wa baadhi ya wadau kuhusu wajibu wao kisheria ndiyo sababu ya kuanza kwa kampeni ya kutoa elimu, ambayo inalenga kufungua macho ya wauzaji na wasambazaji juu ya umuhimu wa virutubishi kama sehemu ya viwango vya ubora.

“Bidhaa yoyote inayokosa virutubishi ni tishio kwa afya ya mlaji kwa hiyo tunataka kuona kila mfuko wa unga unaouzwa sokoni umezingatia vigezo hivi,” ameongeza

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wasambazaji wa Nafaka Mkoa wa Dar es Salaam, Emmanuel Benjamin, amesema kuwa elimu hiyo imekuja kwa wakati muafaka na kupongeza TBS kwa kuwaleta wadau pamoja ili kufikia malengo ya pamoja ya afya na ubora wa bidhaa.

Tablan Shaban naye ni mshiriki wa mafunzo hayo amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuchukua hatua stahiki katika biashara zao na kuhakikisha wanasambaza unga unaokidhi viwango vya afya vilivyowekwa.

Kampeni hiyo inaendelea katika vituo vya Temeke, Ubungo na Kinondoni hadi Septemba 16, 2025, na inatarajiwa kufanyika pia katika mikoa mingine nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuboresha lishe kupitia bidhaa za viwandani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here