Na Esther Mnyika, Zanzibar
MGOMBEA wa Urais Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa wagombea wa vyama vya siasa 11 vilivyopitishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufanya kampeni za kistaarabu na kuepukana na lugha za matusi, kulinda amani.

Dk.Mwimyi ametoa wito huo Septemba, 12 mwaka 2025, Mjini Unguja Zanzibar, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
“Tuendelee kudumisha amani na utulivu , tushindane kwa kwa sera na wakiwa na sera watakuwa wanawasema watu wasiharibu mgawanyiko wa nchi, tuhubiri amani wanao hubiri chuki tuachane nao,” amesema Dk.Mwinyi.

Amesisitiza kuwa wasisahau kuwa yeye bado ni Rais hivyo waendelea kudumisha amani zaidi kwa sababu hakuna maendeleo bila amani hivyo wafanye kampeni za kistaarabu.
Katika hatua nyingine, Dk.Mwinyi alitumia nafasi hiyo kuwasilisha makadirio ya sera pamoja na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake wa awamu ya kwanza.
Aligusia maeneo mbalimbali muhimu kwa ustawi wa Zanzibar, yakiwemo viwanda, bandari, kilimo, na hasa ajenda yake kuu ya uchumi wa buluu — sekta ambayo amekuwa akiipa kipaumbele kikubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Katika sekta ya viwanda, hatua zimechukuliwa kuanzisha maeneo maalum ya viwanda vidogo na vya kati na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kwa kutoa motisha mbalimbali.
Amesema atafufua viwanda ambavyo vilishakufa na kufanya uwekezaji na uchumi wa Zanzibar kuimalika kwa kupata wawekezaji ambao watawekeza katika kiwanda cha nguo ambacho kitauuza ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wa bandari, kazi ya upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Malindi inaendelea na ni sehemu ya mpango wa kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji wa kimataifa.

Kilimo, ambacho ni chanzo kikuu cha ajira kwa wananchi wengi wa Zanzibar, kimepatiwa msukumo kupitia usambazaji wa pembejeo, elimu kwa wakulima, na kuimarisha masoko ya mazao.
Kuhusu uchumi wa buluu, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa kuna mafanikio makubwa katika uvuvi wa kisasa, ufugaji wa samaki, na uhifadhi wa mazingira ya baharini.
MIPANGO YA AWAMU YA PILI
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, Rais Dk. Mwinyi alikiri kuwa bado kuna miradi muhimu ambayo haijakamilika kutokana na changamoto mbalimbali, zikiwemo za kifedha na kiutendaji.

Hivyo, ametaja mikakati mipya ya kuimarisha utekelezaji endapo atapewa ridhaa na wananchi kuongoza kwa awamu ya pili.
“Tutahakikisha kuwa tunakamilisha miradi yote ambayo haijakamilika, lakini pia tutaibua mipango mipya yenye kuendana na mahitaji ya sasa ya wananchi wetu. Uchumi wa buluu utaendelea kuwa nguzo yetu kuu ya maendeleo,” amesema Dk.Mwinyi.