Na Florah Amon, Dar es Salaam.
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) inadai zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kutoka kwa wapangaji wa nyumba zake ambao hawajalipa kodi ya pango kwa zaidi ya miezi mitatu na kuendelea.

Pia TBA imetangaza kuanza operesheni maalum ya kuwaondoa wadaiwa hao kuanzia Oktoba 1, 2025.
Akizungumza leo Septemba 12, 2025, jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu TBA, Arch.Daud Kondoro, amesema deni hilo linatokana na malimbikizo ya kodi kutoka kwa watumishi wa umma, taasisi za serikali, pamoja na wapangaji wa biashara walioko katika nyumba na maeneo yanayomilikiwa na TBA katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
“Wadaiwa ambao hawatalipa madeni hayo ndani ya muda uliotolewa wataondolewa kwenye nyumba za wakala au maeneo waliyopangishwa pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria hakutakuwa na muda wa ziada wa kulipa madeni hayo, hivyo tunaomba wadaiwa kuhakikisha wanalipa madeni yote katika muda uliotolewa,” amesema Arch.Kondoro.

Amesema kuwa wadaiwa wote waliochelewa kulipa kodi zao wametakiwa kuhakikisha wanalipa madeni yote yaliyolimbikizwa kabla ya Septemba 30, 2025.
Amesisitiza kuwa baada ya muda huo, TBA itaanza rasmi operesheni ya kuwaondoa wote waliokaidi kulipa madeni hayo.
Aidha amesema kuwa hatua hiyo inalenga kudhibiti upotevu wa mapato na kuhakikisha kuwa nyumba na maeneo ya serikali yanatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi wote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Miliki, Said Mndeme, amesema kuwa mikoa inayoongoza kwa madeni sugu ni pamoja na mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma, kutokana na kuwa na idadi kubwa ya nyumba za TBA na wapangaji wengi.
Mndeme ameongeza kuwa tayari notisi zimeshatolewa kwa wadaiwa wote katika mikoa hiyo na mingine, na kwamba utekelezaji wa kuwaondoa utakuwa wa nchi nzima kwa wale wote watakaoshindwa kulipa kabla ya tarehe ya mwisho.

Aidha, ametoa wito kwa wapangaji wote wenye madeni kuhakikisha wanalipa kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kuondolewa kwenye nyumba au maeneo ya serikali wanayoyapangisha.
TBA imesisitiza kuwa hatua hii ni ya mwisho na haitarajii kurefusha muda wa malipo kwa wapangaji ambao watashindwa kutekeleza agizo hilo ndani ya muda uliotolewa.