Home BIASHARA Dk. Mwinyi aahidi ajira zaidi ya 350,000 kwa vijana Zanzibar

Dk. Mwinyi aahidi ajira zaidi ya 350,000 kwa vijana Zanzibar

Na Esther Mnyika, Lajiji- Zanzibar

Mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuendeleza zaidi miradi na sera alizozianzisha katika awamu yake ya kwanza ya uongozi, huku akiahidi kuvuka lengo la Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2030 la kuzalisha ajira 350,000 kwa vijana.

Akizungumza Septemba 13, 2025, katika uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Unguja, Dk. Mwinyi alisema mwelekeo wa uchumi wa Zanzibar kwa sasa ni mzuri, hali inayoipa serikali nafasi ya kutekeleza kwa ufanisi ajenda ya kukuza ajira na uwekezaji.

“Uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 7.4, tunaenda vizuri, na miaka mitano ijayo utaimarika zaidi. Uwekezaji unaoendelea sasa, ikiwemo viwanda vinavyojengwa, vitazalisha ajira nyingi hususan kwa vijana,” alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema ataongeza mafungu ya fedha kwenye mikopo isiyo na riba inayotolewa na serikali, pamoja na kuimarisha hifadhi ya chakula, mafuta na gesi. Alisisitiza kuwa maendeleo anayoyasimamia hayana upendeleo wa kijinsia au kijiografia, bali yanalenga kuwanufaisha wananchi wote wa Pemba na Unguja.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba, Dk. Mohamed Shein, alisema kukopa kwa ajili ya maendeleo ni utaratibu wa kisasa unaotumika hata na mataifa makubwa duniani, akibainisha kuwa hatua zinazochukuliwa na Dkt. Mwinyi zinapaswa kuungwa mkono badala ya kubezwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here