*Asisitiza juu ya uchumi wa buluu
Na Esther Mnyika, Zanzibar
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuimarisha uchumi wa buluu kupitia sekta za uvuvi, kilimo cha mwani na karafuu.
Akihutubia Septemba 15, 2025, mamia ya wakazi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika viwanja vya Gombani ya Kale, ambapo kulifanyika uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM kwa upande wa Pemba, Dk. Mwinyi alisema Serikali ya CCM imejipanga kuhakikisha kilimo cha mwani na shughuli za uvuvi vinakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi, hasa wa Pemba.
“Mwani wote unaozalishwa hapa Pemba utanunuliwa na Serikali na utaongezewa thamani ili wakulima wapate faida kubwa. Tumeshakamilisha kiwanda cha Marangu na mashine tayari zimewasili, hivyo hakutakuwa na changamoto ya soko,” alisema Dk. Mwinyi.
Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kugawa maboti kwa wavuvi na wakulima wa mwani sambamba na kutoa mikopo isiyo na riba kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa samaki na mwani.
Aidha, aligusia changamoto zinazowakumba wakulima wa karafuu, hasa wasiokuwa na uhakika wa umiliki wa mashamba yao. Aliahidi kuwa Serikali itaanza kuwapatia hati miliki wakulima wote wa karafuu ili waweze kuyatunza mashamba yao kwa ufanisi na kuongeza uzalishaji.
“Kuna mashamba ya eka ambayo yakifika msimu hukodishwa kwa watu wengine na wakulima wa awali wanakosa motisha ya kuyaendeleza. Tumeshaanza kutoa hati miliki ili mashamba haya yawe rasmi mali ya wakulima, na yatunzwe vizazi kwa vizazi,” amesisitiza.
Pia alieleza dhamira ya Serikali kuimarisha sekta ya utalii kama sehemu ya uchumi wa buluu, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha Pemba inapata utalii wa kimataifa wa hadhi ya juu.
“Tunataka utalii wa Pemba uwe wa kipekee, wenye thamani kubwa. Sekta hii tutawekea utaratibu maalumu – hoteli zitakazojengwa ziwe za kiwango cha nyota tano, zinazojali mazingira. Kwa sasa tuna uwanja wa ndege wa kimataifa, hivyo hakuna kizuizi kwa Pemba kufunguka kiutalii,” alisema.
Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa utekelezaji wa yote hayo ni sehemu ya Ilani ya CCM na kwamba chama hicho kiko tayari kuendeleza mafanikio ya Serikali ya awamu iliyopita kwa asilimia 100.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amewahakikishia Wazanzibari kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa usalama na amani.
Alisema kampeni za CCM zitakuwa za nyumba kwa nyumba, kwa kutoa ushirikiano na kuhakikisha kila mmoja anapiga kura kwa mujibu wa haki yake ya kikatiba.
“Nataka CCM ishinde kwa kishindo. Nimesikia upande wa pili wameanza kuunda vikundi vya malalamiko, lakini mwaka huu Wazanzibari na Wapemba hawataki hayo. Tuendelee na kampeni za kistaarabu,” alisema.



