Home KITAIFA Dk. Mwinyi: Pemba inakwenda kufunguka kupitia bandari, Airport ya kimataifa

Dk. Mwinyi: Pemba inakwenda kufunguka kupitia bandari, Airport ya kimataifa

Na Esther Mnyika, Zanzibar

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi, amesema Pemba ipo mbioni kufunguka kiuchumi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa bandari na uwanja wa ndege wa kimataifa, ambao mkandarasi anatarajiwa kukabidhiwa mwezi huu kuanza ujenzi.

Akizindua kampeni za CCM kwa upande wa Pemba Septemba 15, 2025, katika viwanja vya Gombani ya Kale, Mkoa wa Kusini Pemba, Dk. Mwinyi alisema miradi hiyo itakuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kisiwani humo.

“Ndugu zangu, hakuna sababu kwa nini Pemba isifunguke. Septemba 25 tunamkabidhi mkandarasi kuanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba. Pia kuna bandari zimejengwa na nyingine zinaendelea kujengwa. Pemba itafunguka,” alisema Dk. Mwinyi.

Mbali na uwanja wa ndege, alisema mkandarasi huyo pia ataanza ujenzi wa barabara ya Chakechake–Mkoani, ambayo itakuwa kiunganishi muhimu cha usafirishaji kati ya bandari ya Mkoani na maeneo mbalimbali ya Pemba.

Aidha, alisema bandari za Mkoani na Shumba zinatarajiwa kubadilisha kabisa uchumi wa Pemba kwa kuwa meli kubwa za kimataifa zitakuwa zikishusha mizigo yake moja kwa moja katika bandari hizo.

Karafuu na mwani
Akizungumzia kilimo cha karafuu, Dk. Mwinyi alisema licha ya zao hilo kuwa kuu kisiwani humo, wananchi walikata tamaa na kuyatelekeza mashamba kutokana na changamoto mbalimbali.

“Zao letu la karafuu limekuwa likipata changamoto, na imefika hatua wakulima wakayatelekeza mashamba. Sasa nawaambia kila mwenye shamba alishikilie na kulitunza, maana neema inakuja,” alisema.

Kuhusu zao la mwani, alisema Serikali itaimarisha sekta hiyo kwa kuwapatia wakulima vifaa vya kisasa na kwamba tayari kiwanda cha Manangwe kimejengwa kwa ajili ya kuchakata mwani.

“Tutaendelea kuwapa wakulima vifaa vya kisasa. Zao lote tutalinunua na kuchakata kiwandani, kwa hiyo hakutakuwa na tatizo la soko. Haya ndiyo tunakwenda kuyamalizia,” alisema.
Dk. Mwinyi alisema endapo CCM itapewa ridhaa ya kuunda Serikali katika awamu ijayo, kisiwa cha Pemba kitashuhudia mageuzi makubwa ya kiuchumi.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba kura wananchi wa Pemba ili chama hicho kimalizie miradi iliyoanza, huku akiwakosoa wapinzani kwa kukosa sera zenye mashiko.

“Msidanganywe na chochote, kwanza hao hawana sera. Hata haya tuliyoyasema hapa tayari mmeyasikia wakiyarudia,” alisema huku wananchi wakijibu kwa sauti ya pamoja: “Hapana.”

Awali, akimkaribisha Dk. Mwinyi na kumwombea kura, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema Serikali ya awamu ya nane imefanya mambo makubwa yasiyowahi kufanyika na hivyo inastahili kuungwa mkono.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here