Na Esther Mnyika, Gazetini
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema chama chake kimejipanga kumaliza changamoto ya ajira kwa vijana endapo atachaguliwa kuendelea kuongoza katika awamu ya pili.
Akizungumza Septemba 16, 2025 katika mkutano na waendesha bodaboda, wakulima wa viungo na wajasiriamali wa Shehia ya Mndo, Wilaya ya Magharibi A, Dk. Mwinyi alisema Serikali itatoa nafasi za ajira katika sekta za elimu, afya na nyinginezo sambamba na mafunzo ya kuwawezesha vijana kujiajiri.
Ameeleza kuwa kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), programu za utoaji wa mitaji, mafunzo, maandalizi ya masoko na vitendea kazi zitaimarishwa ili kuunga mkono juhudi za wajasiriamali.
Akigusia kilimo cha viungo, aliahidi kutenga maeneo maalum, kuwapatia wakulima pembejeo na masoko ya uhakika. Aidha, Serikali itatoa mikopo kupitia vikundi vya ushirika kusaidia waendesha bodaboda na wajasiriamali wadogo.
Dk. Mwinyi aliwahimiza wananchi kuendelea kukiamini CCM akisema ndicho chama pekee chenye dhamira ya kudumisha amani na kuleta maendeleo Zanzibar.