Home KITAIFA Muungano ni udugu wa damu, tutaulinda kwa bidii-Dk. Samia

Muungano ni udugu wa damu, tutaulinda kwa bidii-Dk. Samia

Na Mwandishi Wetu, Lajiji

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na kudumisha amani, uhuru, umoja na utulivu nchini endapo atachaguliwa tena kuongoza Watanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza leo Jumatano, Septemba 17, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Kajengwa, Makunduchi Visiwani Zanzibar, Dkt. Samia alisema Muungano ni urithi mkubwa ulioachwa na waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Amani Abeid Karume, hivyo unapaswa kuendelezwa kwa vizazi vijavyo.

“Naweza kusema Muungano wetu sasa umekuwa Muungano wa udugu wa damu zaidi kuliko vigezo vingine vyote. Pamoja na Muungano wetu tumeweza kulinda Uhuru na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, na hali kadhalika kudumisha umoja, amani na utulivu nchini. Hizi ndizo tunu kuu na za msingi kwa maendeleo ya nchi yetu na niwaambie tutazilinda kwa bidii zetu zote,” amesema Dk. Samia.

Dk. Samia ameongeza kuwa tunu hizo zimeijengea Tanzania hadhi ya kipekee Kikanda na Kimataifa, na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia unaoendelea kufungua milango ya fursa za kimaendeleo kwa Watanzania.

Katika kuonesha uthabiti wake wa kuulinda urithi huo, Dk. Samia ameahidi kuanzisha Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kituo hicho kitalenga kuhifadhi historia na misingi ya Muungano pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kujifunza sababu za uwepo wake na mchango wake katika kudumisha mshikamano wa kitaifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here