Home KITAIFA Nimekuja nyumbani kuchota baraka za wazee- Dk. Samia

Nimekuja nyumbani kuchota baraka za wazee- Dk. Samia

Na Mwandishi wetu, Lajiji

Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema amerejea Zanzibar na kuanzia kampeni zake Makunduchi Unguja, sehemu ya asili yake ili pamoja na mambo mengine aweze kupata baraka za Wazee na wanajamii wenzake ili kuweza kuyakabili vyema majukumu yaliyopo mbele yake.

Dk. Samia ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar na mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania kuwa Makamu wa Rais na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye pia Mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Juu ndani ya CCM na mwanamke wa kwanza kupitishwa na Chama hicho kuweza kuwania nafasi ya Urais anayoiwania sasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 17, 2025 kwenye Kampeni zake kwenye Viwanja vya Kajengwa, Dkt. Samia ametumia fursa hiyo pia kuwashukuru wana Jamii wa Makunduchi kwa baraka na maombi yao, akiwaomba pia kuweza kumchagua katika uchaguzi mkuu ujao.

“Tumejiamini na tumepata ujasiri wa kurudi tena kwenu ndugu wananchi na kuomba ridhaa na dhamana ya kuongoza tena nchi yetu kwa miaka mitano ili tuipeleke kwenye mafanikio zaidi. Chama Cha Mapinduzi tumeweza, tumefanya, tuliahidi tukatekeleza, tunaahidi makubwa zaidi na nataka niwaambie tutatekeleza, tunajiamini na tuna kila sababu ya kuja kwenu kwa ujasiri kabisa kuwaambia tunaweza, tupeni, tutatekeleza,” amesema Dk. Samia.

Tangu kuzinduliwa kwa kampeni za Chama hicho Agosti 28, 2025, Dk. Samia pamoja na Mgombea mwenza wake Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi wamekuwa wakitembea na kufanya mikutano kwenye maeneo mbalimbali nchini, huku kukishuhudiwa wingi mkubwa wa wananchi kwenye mikutano yao, suala ambalo Wanasiasa hao wamesikika wakisema wingi huo wa watu ni dhihirisho la Chama na Wagombea wake kukubalika kutokana na uwezo wao na utekelezaji mkubwa wa ahadi walizoahidi kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/25.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here