Home KITAIFA Samia; Amani na utulivu wa Tanzania ni jambo muhimu kuliko yote

Samia; Amani na utulivu wa Tanzania ni jambo muhimu kuliko yote

Na Mwandishi Wetu, Lajiji

Akiwa kwenye Kijiji cha Kajengwa, Makunduchi Unguja Visiwani Zanzibar, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan amewatoa wasiwasi Watanzania akiwahakikishia kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu katika kuilinda Tanzania na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na salama.

Dk. Samia akirejea ahadi yake wakati anajitambulisha kwa Watanzania mara baada ya Chama chake kumpa ridhaa ya kuwania nafasi ya Urais, akiwa mwanamke wa kwanza kupewa nafasi hiyo katika Historia ya Chama hicho, amesema amelazimika kuyasema hayo mara baada ya Wazee wa Pemba kumuomba kusimamia amani na utulivu katika uchaguzi huo Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi Mkuu, ninaowaomba sana twende tudumishe amani na utulivu. Uchaguzi si vita, uchaguzi ni tendo la kidemokrasia ni watu kwenda kwenye utaratibu uliowekwa, kuweka kura zetu, rudi nyumbani katulie ili nchi ibaki salama. Si muda wote kushika silaha kunaleta suluhu ya maana, niwaombe sana ndugu zangu amani na utulivu wa nchi yetu ni jambo muhimu kuliko jambo lolote. Hutaki kishindo kapige kura rudi nyumbani tulia,” amesema Dk. Samia.

Dk. Samia yupo Visiwani Zanzibar kwenye ziara zake za Kampeni, ambapo awali pia amesisitiza kuwa ikiwa Watanzania watampa ridhaa ya kuongoza serikali atahakikisha pia analinda kwa bidii zake zote tunu za Taifa ambazo ni amani, umoja na mshikamano kama sehemu ya kuenzi jitihada zilizofanywa na waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Amani Abeid Karume.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here