-Asema uchaguzi siyo vita ni tendo la demokrasia
Na Mwandishi Wetu, Lajiji
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa uchaguzi siyo vita bali ni tendo la demokrasia.
Akihutubia leo, Jumatano Septemba 17, 2025, katika kijiji cha Kajengwa, Makunduchi, Visiwani Zanzibar, Dkt. Samia amesema amani ni msingi wa maendeleo ya Taifa na inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote, hususan wakati huu wa uchaguzi.
“Ndugu zangu, tunaingia kipindi cha uchaguzi. Mwanzo nilipokuja kujitambulisha, ahadi kubwa niliyoitoa ni kuifanya Tanzania iwe na amani na utulivu. Sasa tunapoelekea Uchaguzi Mkuu, nawaomba sana tudumishe amani na utulivu. Uchaguzi si vita, ni tendo la demokrasia. Nenda weka kura yako, kisha rudi nyumbani ukatulie ili nchi ibaki salama,” amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ameonya dhidi ya vitendo vya vurugu na matumizi ya silaha za aina yoyote, akisema havileti suluhisho la maana kwa Taifa. Amesisitiza kuwa utulivu na mshikamano wa kitaifa unapaswa kupewa kipaumbele na kila Mtanzania.
Aidha, Dkt. Samia amesema vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama na ya amani, Bara na Visiwani.



