Home BIASHARA Dk. Samia aahidi kukuza uchumi, ajira na utawala bora

Dk. Samia aahidi kukuza uchumi, ajira na utawala bora

Na Esther Mnyika, Zanzibar

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo serikali ya chama hicho itaendeleza juhudi za kukuza uchumi wa nchi, kuongeza kipato cha wananchi na kudumisha misingi ya demokrasia pamoja na utawala bora.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 18, 2025 katika Viwanja vya Hamburu, Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Samia aliwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa mahudhurio makubwa na mapokezi waliyoyatoa kwa CCM.

“Kwa mambo yaliyofanyika na bashasha tuliyoiona hapa Zanzibar hatuna wasiwasi na ushindi wa CCM, lakini uungwana unatutaka tuje tuwaombe mtuchague kwa mara nyingine. Tuna ujasiri wa kuomba tena kura kwa mwaka 2025/30 kwa sababu tumefanya mambo makubwa na tunaamini tutaweza kufanya makubwa zaidi,” alisema.

Dk. Samia pia aliahidi kuimarisha ustawi wa jamii, kulinda amani na usalama wa Taifa, pamoja na kujenga uchumi unaojitegemea kupitia uwezeshaji wa wananchi. Alibainisha kuwa serikali itajipanga kuandaa mazingira bora kwa vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato.

Aidha, aliweka msisitizo kwamba ajenda hiyo itaendana na kaulimbiu ya kampeni zake za mwaka huu: “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here