Na Mwandishi wetu, Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Pemba kuwa Serikali itaendelea kuweka uwiano sawa wa miradi ya maendeleo kwa Unguja na Pemba.

Akizungumza leo Septemba, 24 2025 na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Soko la Chakechake wa Mkoa wa Kusini Pemba Dk. Mwinyi amesema miradi mbalimbali imekuwa ikitekeleza kwa usawa ikiwemo Sekta za miundombinu, elimu, afya na nyenginezo.

Amesema Serikali itaendelea kulinda na kuimarisha soko la asili la Chakechake ili libakie na uasili wake huku ikipanga kujenga soko jipya la kisasa.
“Suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa Serikali ijayo itaongeza mara dufu fedha za uwezeshaji ili kuhakikisha kila mjasiriamali anapata mkopo bila kuachwa nyuma,” amesema Dk. Mwinyi.

Pia amewahakikishia wafanyabiashara ambao hawajapata mkopo unatolewa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(ZEEA) watapata endapo akipata ridhaa ya kuiongoza tena Zanzibar.
“Ninawahakikishieni kwamba wale ambao hawajapata wataweza kupata safari hii lakini wale ambao wamepata wakarejesha watakapopata tena watapata kiwango kikubwa zaid kwa sababu watakuwa wameonyesha uwezo wao wa kurejesha mikopo wanayoipata,” amesema Dk. Mwinyi.

Amesema serikali ina mikopo aina mbili mikopo ya serikali kuu na mikopo inayotokana na mabaraza ya miji na kwamba kwa sasa imeunganishwa pamoja kupitia ZEEA ili kuwafikia zaidi wananchi.

Ameongeza kuwa Serikali itafanyia kazi kwa kina suala la msururu wa kodi na kuweka utaratibu wa kodi nafuu kwa wafanyabiashara.