Na Mwandishi wetu, Mtwara
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara ili kuunganisha Ndanda na Masasi kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 24, 2025, Ndanda, wilayani Masasi, Dkt. Samia alisema Serikali itaendelea kuboresha barabara kwa viwango tofauti kulingana na mpango wa maendeleo.

“Tutaboresha barabara nyingine kwa kiwango cha changalawe na nyingine kwa kiwango cha lami. Ile barabara iliyoombwa tutaangalia kama ipo kwenye ilani na tutaiweka kwa kiwango cha lami. Lengo letu ni kuunganisha Ndanda na Masasi ili mazao ya kilimo yaweze kusafirishwa kwa kasi,” amesema Dkt. Samia.

Aidha, ameibainisha kuwa Serikali itaendelea kutoa mbolea kwa ruzuku na kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao ya biashara kwa wingi ili kuinua uchumi wa wananchi.