Na Mwandishi wetu
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hasara na Maafa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi (Loss and Demage Fund) Ibrahima Diong, mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.

Mazungumzo hayo yamelenga masuala mbalimbali yahusuyo mabadiliko ya tabianchi na athari zake kwa mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania. Pia ukusanyaji wa fedha kwaajili ya mfuko huo na hivyo kuziunga mkono nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania ambazo zinaendelea kuchukua hatua ya kukabiliana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi licha ya uhaba wa fedha.
Mfuko Mfuko wa Hasara na Maafa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi (Loss and Damage Fund), ni utaratibu wa fedha ulioundwa ili kutoa msaada wa kifedha kwa nchi zinazoendelea ambazo zinakabiliwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Athari hizo ni pamoja na majanga ya asili kama mafuriko, ukame, na kupanda kwa kina cha bahari.

Malengo ya mfuko huo ni pamoja na kusaidia nchi zilizohatarini zaidi, kama vile nchi ndogo za visiwa na zile zenye mapato ya chini, ambazo zimeathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi ingawa zimechangia kidogo katika uzalishaji wa gesi chafu. Pia kufidia hasara zisizoepukika, yaani athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo haziwezi kuepukwa kupitia hatua za kukabiliana nazo au za kupunguza athari.
Malengo mengine ni pamoja na kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa, kuhamisha jamii zilizo hatarini, na kurejesha ardhi ya kilimo au maeneo ya pwani.

Mfuko huo ulianzishwa rasmi kwenye Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) huko Misri mwaka 2022, baada ya miongo kadhaa ya majadiliano. Katika mkutano wa COP28 Dubai, nchi wanachama zilikubaliana kuanza kuutekeleza mfuko huo.