Home SIASA Dk. Samia aahidi kufanyia kazi hitaji la bandari kavu Korogwe

Dk. Samia aahidi kufanyia kazi hitaji la bandari kavu Korogwe

Na Mwandishi wetu, Tanga

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema alipokea ombi la ujenzi wa bandari kavu Old Korogwe, Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, akiahidi kulifanyia kazi ombi hilo ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali hapo Oktoba 29, 2025.

Dk. Samia ameeleza hayo wakati aliposimama kwenye Viwanja vya Stendi Korogwe leo Septemba 30, 2025 kwaajili ya kuomba kura kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akiahidi pia kujenga barabara ya Soni- Bumbuli- Dindira- Korogwe kwa kiwango cha lami kwa urefu wa Kilomita 74.

Pia ameahidi ujenzi wa barabara nyingine ya Old Korogwe- Kwa Mndolwa- Magoma- Bombo Mtoni- Mabokweni kwa urefu wa Kilomita 128, akisema lengo ni kuifungua zaidi Wilaya hiyo ili wananchi wapate urahisi katika shughuli za usafiri na usafirishaji.

“Ndani ya Korogwe hapa kunapita mradi mkubwa wa kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Chongoleani kwahiyo hapa napo tunakwenda kujitahidi mradi huu ukamilike haraka tukijua kwamba korogwe ni kituo muhimu na kuna ajira zitapatikana kutokana na mradi huo na fursa nyingine nyingi za kiuchumi,” amesema Dk. Samia.

Amesema serikali ya chama chake itaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya barabara, elimu na afya katika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, iwapo wananchi watakiamini tena kuongoza nchi kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

CCM imeweka mpango wa kujenga barabara kuu mbili kwa kiwango cha lami zenye urefu wa zaidi ya kilomita 200. Tutajenga barabara ya Soni – Bumbuli – Dindira – Korogwe yenye urefu wa kilomita 74 na pia barabara ya Old Korogwe – Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Mabokweni yenye urefu wa kilomita 127.69,” amesema.

Ameongeza kuwa serikali pia itatekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege kwenye barabara ya Msambiazi – Lutindi – Kwabuluu ili kurahisisha usafiri na biashara ndani ya wilaya.

Kuhusu sekta ya elimu, Dk. Samia amesema CCM imedhamiria kujenga madarasa 560 Korogwe, hatua itakayopunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza upatikanaji wa elimu bora.

Katika sekta ya afya, amesisitiza kuwa miradi ya kuboresha zahanati na vituo vya afya itaendelea kutekelezwa ili wananchi wa Korogwe wapate huduma bora karibu na makazi yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here