Na Mwandishi wetu
KESI ya Waziri Mkuu wa zamani wa Mali, Moussa Mara imeanza kusikilizwa rasmi katika Mahakama ya uhalifu wa Mtandao katika Mji Mkuu wa Bamko siku ya jana Jumatatu.

Mara ameshtakiwa kwa kudhoofisha uaminifu wa serikali, kupinga mamlaka halali, na kuchochea machafuko ya umma kufuatia maoni aliyoyatoa mwezi Julai kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuwatembelea viongozi wa upinzani waliozuiliwa jela.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X zamani Twitter, alionyesha mshikamano na wapinzani hao, akiwaelezea kama wafungwa wa dhamiri na kuongeza kuwa ziara zake zilikuwa za kuhakikisha kuwa mwaliko wa matumaini haufifii ndani yao.
“Kadiri usiku unavyoendelea, jua litachomoza bila shaka. Na tutapigana kwa njia zote ili hilo lifanyike, na haraka iwezekanavyo,” aliongeza.
Mara ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu kwa miezi tisa muongo mmoja uliopita, hivi karibuni amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya kijeshi.Wanajeshi hao, wakiongozwa na Jenerali Assimi Goita, waliingia madarakani kufuatia mapinduzi mawili mwaka wa 2020 na 2021.
Aliteuliwa kuwa rais wa mpito mwaka 2021, akiahidi uchaguzi mwaka uliofuata, lakini Mei mwaka huu, alivifuta vyama vyote vya siasa kufuatia maandamano nadra dhidi ya serikali.
Mnamo Julai, Goita aliidhinisha sheria inayompa mamlaka ya urais ya miaka 5, ambayo yanaweza kubadilishwa mara nyingi kumruhusu kukaa madarakani bila uchaguzi wa kidemokrasia kuitishwa.