Home SIASA Tutakuza utalii wa Mkoa wa Manyara-Dk.Samia

Tutakuza utalii wa Mkoa wa Manyara-Dk.Samia

Na Mwandishi wetu, Manyara

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kutangaza na kuendeleza vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani Manyara kama sehemu ya kufikia ahadi ya Chama chake ya kutaka idadi ya watalii wa ndani na nje ya Tanzania kufikia Milioni nane mwaka kabla ya mwaka 2030.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 04, 2025 Dk.Samia wakati wa Mkutano wake wa Kampeni Babati Mjini kwenye Viwanja vya CCM Sabasaba, akiita hifadhi ya Tarangire na Ziwa Manyara kama Vivutio vikuu Mkoani humo na akiahidi kuviendeleza pamoja na kujenga barabara zinazoenda kwenye Vivutio hivyo kama sehemu ya kukuza pato na uchumi wa mwananchi na wa Mkoa huo.

Ameeleza kufahamu mgogoro wa wananchi wa Simanjiro na Kiteto na pori la Mkungunero, kutokana na wananchi kuingia ndani ya pori hilo kufuata huduma ya maji na hivyo kuiagiza Wizara ya maji kuhakikidha Vijiji vyote vya kuzunguka pori hilo vinapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao.

“Naahidi pia kushughulikia kero ya wanyamapori kutoka kwenye maeneo ya hifadhi na kuvamia mashamba ya wakulima na kudhuru wananchi, akisema serikali ya awamu ya sita imeanza jitihada mbalimbali za udhibiti wanyamapori hawa ikiwemo ujenzi wa vituo vya askari wanyamapori pamoja na kuwafunga wanyama hawa vifaa maalumu ya utambuzi pale wanapokuwa wametoka nje ya hifadhi ili kuzijulisha mamlaka kuhusu kutoka kwao,” amefafanua.

Dk. Samia amesema Ilani ya Chama chake anayoinadi sasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imemtaka kuimarisha mawasiliano Vijijini pamoja na kukuza matumizi ya TEHAMA kama sehemu muhimu ya kufikia maendeleo.

Amebainisha pia mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta hiyo kwa awamu ya kwanza ya serikali ya awamu ya sita akisema wameongeza upatikanaji wa huduma za simu za kiganjani kutoka asilimia 83 hadi 93 ikitokana na ujenzi wa ujenzi wa minara ya simu 5 kwa Wilaya ya Hanang, 17 Simanjiro pamoja na minara 21 kwenye Wilaya ya Kiteto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here