Home SIASA Tuwakatae wanaoichafua nchini kushusha heshima ya Tanzania Kimataifa-Dk.samia

Tuwakatae wanaoichafua nchini kushusha heshima ya Tanzania Kimataifa-Dk.samia

Na Mwandishi wetu, Mwanza

MGOMBEA wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kulinda na kuheshimisha jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani na nje ya nchi, huku pia akiwahimiza watanzania kuwakataa wale wote wanaodhohofisha na kuchafua heshima ya Tanzania Kimataifa.

Dkt. Samia ameyasema hayo leo Oktoba 07, 2025 akiwa mbele ya maelfu ya wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wa Wilaya za Buchosa na Sengerema Mkoani Mwanza, Kampeni zake za Uchaguzi Mkuu Mkoani Mwanza .

Amesema Tanzania itaheshimisha ikiwa itaendelea kufuata misingi ya haki, kufanya chaguzi bila vurugu na zogo sambamba na kufuata sheria zetu wenyewe pamoja na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia Kimataifa.

“La mwisho tutakalolifanya ni kuheshimisha jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya nchi na nje ya nchi. Tutaheshimisha nchi yetu kwa kuendeleza amani, kufanya chaguzi bila mavurugu, bila matatizo, bila zogo. Lakini pia tutaheshimisha nchi yetu kama tunafuata sheria zetu wenyewe, kila mtu anapata haki yake na mambo kama hayo na nje ya nchi ni kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia ambao mpaka hatua tuliyoifikia, jina letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zuri sana, linaheshimika sana nje ya Tanzania.

Hayo ndio mambo ambayo nchi yenu, serikali yetu mkitupa ridhaa tunaenda kuyaendeleza. Tunataka kuhakikishia pia kila Mtanzania yupo karibu na huduma za afya na anatibiwa bila shida, kila Mtanzania anapata maji safi na salama, kila Mtanzania anapata fursa za elimu bila kujali hadhi yake, lakini la pili ni sekta zote zinazokuza uchumi wetu tunaziangalia kwa karibu.

“La tatu ni kuheshimisha jina letu. Na hapa wapo watanzania ambao kila wakiona jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaheshimika duniani, kazi yao ni kushusha heshima ya nchi yao nawaomba tuachane nao, tuwaache waende kivyao vyao, hao sio wenzetu,” amesema Dk. Samia Suluhu.

Amesisitiza kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi haitokuwa na mwisho katika kutoa huduma za maji, elimu na afya kwa Watanzania, akitanabaisha kuwa huduma hizo ni endelevu kulingana na ongezeko la idadi ya watu na mahitaji.

Ameongeza kuwa kamwe Chama chake hakitokoma katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hizo za kijamii kwa karibu zaidi, kwa viwango na ubora.

Ametolea mfano changamoto na mahitaji ya Maji Misungwi Mjini, akisema serikali yake imetoa Bilioni 888 kupanua mtandao wa maji wa Kilomita 38 ambapo matenki mawili yenye ujazo wa Lita 150,000 na lingine la ujazo wa lita 90, 000 yamejengwa kwenye Kata ya Misungwi na Igokelo ili kupeleka maji kwenye maeneo ya mwinuko ya Mbela, Mwambola, Ng’ombe, Iteja na Mwamanga.

Dk. Samia amesema mradi huo tayari umefikia asilimia 87 ya utekelezaji wake, akibainisha kuwa kukamilika kwake kutanufaisha wananchi zaidi ya 22, 482.

Amezungumzia pia utekelezaji wa miradi ya Maji Vijijini, akisema serikali yake inatekeleza miradi kumi yenye thamani ya Bilioni 65 ikiwemo mradi mkubwa wa Ikiliguru utakaohudumia Vijiji 19 vya Kata za Usagara, Ukiliguru na Kolomije ambapo tayari tanki la ujazo wa lita Milioni moja na laki tano limekamilika kwenye Kata ya Usagara na lingine la Lita Milioni mbili likiwa linaendelea kujengwa kwenye Kata ya Ukiliguru, mradi ukitarajiwa kunufaisha wananchi 85, 500.

Ameitaja pia miradi ya maji ya Ilijamata utakaohudumia Vijiji 16, akiahidi ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali atasimamia ukamilishaji wa miradi hiyo na kushughulikia ipasavyo changamoto zinazotooana na miundombinu ya usambazaji wa maji kwenye maeneo ya Misungwi na Mkoa wa Mwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here