Na Mwandishi wetu, Shinyanga
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Chimaguli Samamba (54), mkulima na mkazi wa Ugede- Songambele kwa tuhuma za kumuua mke wake kwa sababu ya kuchelewa kurudi nyumbani.

Taarifa iliyotolewa na Polisi imesema Oktoba 8, 2025 katika Kitongoji cha Ugede Kata ya Salawe mwanamke aliyefahamika kwa jina la Moshi John (47) aligundulika kuuawa na mwili wake kufukiwa kwenye shimo lilipo jirani na nyumbani kwake.
Imeelezwa kuwa mnamo Oktoba 1, 2025 majira ya saa 4 usiku, marehemu Moshi aligombana na mume wake kutokana na kuchelewa kurudi kutoka matembezi. Baada ya ugomvi huo, mume wa marehemu alimshambulia kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hadi mke wake kuishiwa nguvu na kufariki dunia.
“Baada ya mtuhumiwa kubaini kuwa mkewe amefariki dunia alichukua mwili wa marehemu na Kwenda kuutupa nje pembeni mwa nyumba yao kwenye shimo lililokuwa likichimbwa kwa matumizi ya choo, na aliufukia mwili kwa udongo,” imeeleza taarifa.
Aidha, taarifa imeeleza kuwa majirani walianza kupata wasiwasi baada kutomwona mwanamke huyo na pia kutokana na tabia ya mwanaume huyo kumpiga mara kwa mara hivyo walianza kufuatilia, na taarifa hizo kufikishwa kwa mwenyekiti wa kitongoji Oktoba 07, 2025 ambaye alifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumhoji, lakini alikana kuhusika na uhalifu huo.
Hata hivyo, Oktoba 8, 2025, mwenyekiti alitoa taarifa polisi na ndipo walipofika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumkamata, na baada ya mahojiano ya awali, mtuhumiwa alikiri kumuua mkewe na kumfukia kwenye shimo la choo.