๐Mpango wa kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali umewezekana
๐ Yaahidi zawadi nono kwa wananchi watakaotoa taarifa za wahujumu kupitia mfumo wa Whistleblower
Na Agnes Njaala, Mkuranga
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) likiendelea na operesheni maalumu ya ukaguzi wa mita katika Kanda ya Mashariki, Mkoa wa Pwani Kusini, limebaini wizi wa umeme katika kiwanda cha SANFU kilichopo eneo la Mwanambaya, Mkuranga, kinachojishughulisha na uzalishaji wa mafuta kwa kutumia matairi ya magari.

Katika ukaguzi huo imethibitika kuwa, mita ya T2 aina ya EDMI iliyofungwa katika kiwanda hiko imekatwa lakili (seal) ambayo kazi yake huwa ni kulinda mita dhidi ya uharibifu kitendo kilichowezesha uchepushaji wa usomaji sahihi wa matumizi halisi ya umeme na kupelekea mtumiaji kulipa bili chini ya kiwango halisi.
Akizungumza Oktoba 07, 2025 , Mhandisi wa Kitengo cha Uthibiti Mapato Makao Makuu , Mposhelei Mwasongo ameainisha kuwa mteja huyo alianza matumizi hayo yasio halali mnamo Disemba 2024 mpaka kukamatwa kwake Octoba 06, 2025 ambapo jumla ya deni lake kwa kipindi hicho chote ni takribani Shilingi Milioni 221,432, 346.56 huku makadirio ya matumizi yake yanaonesha bili yake kwa mwezi alipaswa kulipa zaidi ya milioni 20.

Akifafanua zaidi , Afisa Usalama Mwandamizi TANESCO,Stephen Maganga amesema pamoja na uwekezaji na uzalishaji mkubwa wa kiwanda hicho, Mteja huyo amekuwa akilipa bili ya kiasi cha shilingi 72,000 kwa mwezi ambayo siyo sahihi na hivyo kusababisha hasara ya upotevu wa mapato kwa Shirika na Serikali.
โ Niwaombe wateja wetu na watanzania kwa ujumla mtambue kuwa hili Shirika ni letu sote na tunapofanya hujuma tunaikosesha serikali mapato na kuathiri Shirika katika kuwahudumia wateja wengine wanaohitaji huduma ya umeme,”amesisitiza Maganga.

Ametoa wito kwa wananchi kuendeleza ushirikiano na Shirika kwa kutoa taarifa za wahujumu kupitia mfumo wa kimtandao wa utoaji wa taarifa za siri (Whistleblower) unaopatikana kwenye tovuti ya TANESCO akisisitiza kuwa mfumo huo ni salama katika kulinda usiri wa taarifa zinazotolewa.
Aidha, amesisitiza kuwa zawadi nono zitatolewa kwa watoa taarifa zitakazothibitika kuwa sahihi, kuanzia kiasi cha Shilingi 100,000 hadi Milioni 1, kulingana na aina ya taarifa ikiwa ni hatua ya kuchochea ulinzi wa miundombinu na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa watanzania.
Shirika linasisitiza kuwa zoezi hili ni endelevu nchi nzima likilenga kudhibiti upotevu wa mapato kwa kuwabaini wateja wanaotumia umeme kinyume na utaratibu na kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwemo kusitishiwa huduma, kulipishwa faini, na kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.