Na Mwandishi wetu
ZAIDI ya vituo 200 vya afya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa ikiwa ni matokeo ya moja kwa moja ya migogoro inayoendelea na kuporomoka kwa ufadhili wa kibinadamu.

Tathmini mpya ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu inaonyesha kuwa 80% ya kliniki za Kivu Kaskazini na Kusini, majimbo yaliyoharibiwa na vita, zinafanya kazi bila msaada wowote kutoka nje. Wengi hawana uwezo wa kupata matibabu ya kimsingi ya malaria, VVU, na kifua kikuu.
Mapigano hayo, yanayochochewa na waasi M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, yamefanya iwe vigumu kusafirisha dawa katika mstari wa mbele wa mapigano licha ya uwepo wa vifaa.
Kwa mujibu wa François Moreillon kutoka kamati hiyo ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Wahudumu wa afya wanakimbia na kuwaacha wagonjwa wakifa na maelfu ya maisha hatarini.
Zaidi ya watu 3,000 wameuawa mwaka huu, na milioni 7 wameyahama makazi yao, na hivyo kuzidisha kile ambacho tayari ni moja ya janga mbaya zaidi la kibinadamu ulimwenguni.