Na Mwandishi wetu, Geita
MGOMBEA wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka yake minne madarakani amefanikiwa kuendeleza sekta ya Utalii Wilayani Chato Mkoani Geita ikiwemo Utalii na uhifadhi wa Hifadhi ya Burigi Chato na Utalii wa Kisiwa cha Rubondo.

Ameyasema hayo leo Oktoba 13, 2025 Dk.Samia Wilayani Chato Mkoani Geita wakati wa Mkutano wake wa Kampeni za uchaguzi Mkuu wa Tanzania akieleza pia kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo Wilayani humo ikiwemo ujenzi wa Vizimba 23 na mitumbwi mitano ya kuvulia samaki ili kuongeza uwezo wa uvuvi kwa wavuvi wa Wilaya hiyo.
“Hayati Dk. John Pombe Magufuli (Rais wa awamu ya tano wa Tanzania) alianzisha hifadhi ya Burigi Chato na shughuli za utalii kwenye Kisiwa cha Rubondo na tunapoendelea tumeendelea kutekeleza yale yote aliyoyaacha na sasa tunajenga nyumba za watalii na hoteli ndani ya hifadhi ya Burigi Chato lakini vilevile hoteli ya nyota tano, nyumba za watalii na barabara za ndani ndani ya hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo ambapo haya yote yalikuwa yetu ya pamoja nami nimeyakamilisha,” amesema.

Kwa upande wa sekta ya Kilimo na wakulima Dk. Samia amesema serikali yake ya awamu ya sita imetoa matrekta, ruzuku za mbegu za kilimi, mbolea na pembejeo za kilimo, akiahidi kuendelea kuongeza kasi zaidi na viwango vya utoaji wa ruzuku hizo katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwa Watanzania watampatia ridhaa ya kuunda serikali kupitia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Amezungumzia mafanikio mengine ya serikali yake Wilayani Chato, akisema wamefanikiwa pia kumaliza ujenzi wa kituo cha mabasi Kahumo kinachohudumia mabasi zaidi ya mia moja kwasasa na hivyo kukuza biashara na uchumi wa Chato sambamba na kutoa zaidi ya Bilioni moja kutoka kwenye Mikopo ya Halmashauri kwa Vikundi mia moja vya wanawake, Vijana na wenye ulemavu.