Na Mwandishi wetu, Kigoma
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameahidi kupambana na ufisadi, kusimamia haki, na kuhakikisha Kigoma inakuwa kituo imara cha uchumi kama ilivyokusudiwa.

Zitto ametoa ahadi hizo Oktoba 12, wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Kigoma, akisisitiza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi kwa vitendo.
Amesema atachochea juhudi za kuifanya Kigoma kuwa Kituo cha Biashara na Uchukuzi wa Maziwa Makuu kwa kuimarisha Bandari ya Kigoma, kuhakikisha inaongeza thamani ya mizigo kutoka nchi jirani, na kwamba mikataba yote ya uendeshaji wa bandari inaleta manufaa kwa wananchi wa Kigoma.
“Naahidi p kusimamia kukamilika kwa mradi wa Chelezo cha Ujenzi wa Meli (Shipyard) Katabe–Bangwe, utakaotoa ajira na kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi wa ndani na atahakikisha reli ya SGR inafika Kigoma kwa wakati na kwamba eneo la stesheni litachaguliwa kwa manufaa ya jamii,”‘amesema.
Akizungumzia historia ya uongozi wake wa awali (2015–2020), Zitto alikumbusha mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongozi wa ACT Wazalendo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, akitaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa.
Amesema waliweza kujenga barabara za lami, kuanzisha masoko kama Soko la Jioni la Mzee Menge (Marungu), kuboresha Stendi ya Gungu, kujenga mialo ya wavuvi Kibirizi na kuanza ujenzi wa mwalo wa Katonga. Pia walijenga shule mpya, vituo vya afya, bandari mbili — Ujiji na Kibirizi — na kusukuma ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho.
Aidha, ameahidi kushughulikia kukamilika kwa Soko la Kimataifa la Mwanga na kuimarisha masoko ya jioni ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo. Pia ataharakisha ujenzi wa Soko la Kibirizi, ambalo litakuwa eneo lenye uhai kwa wafanyabiashara wa ndani.
Katika mipango yake, Zitto amepanga kufufua mji wa Ujiji na kurejesha hadhi yake kama kitovu cha biashara kupitia mradi wa Ujiji City, kushughulikia mafuriko katika Forodha ya Ujiji kwa kutumia teknolojia ya fabricated iron bars, na kuhakikisha boti za abiria zinaweka nanga katika Bandari ya Ujiji.
Pia ameahidi kujenga barabara ya Msimba–Ujiji, kuifanya Stendi ya Ujiji kuhudumia wasafiri wa ndani ya mkoa, kukamilisha Mradi wa Umwagiliaji Bonde la Luiche, kujenga daraja juu ya Mto Luiche, na kufungua Soko Kuu la Vyakula Ujiji.