Home KITAIFA Dk. Samia kukomesha tatizo la maji Muleba kwa maji ya Ziwa Viktoria

Dk. Samia kukomesha tatizo la maji Muleba kwa maji ya Ziwa Viktoria

Na Mwandishi Wetu, Kagera
 Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kupitia mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria unaogharimu Sh39.35 bilioni.
 Akihutubia Jumatano, Oktoba 15, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Zimbihile, Samia amesema changamoto ya maji imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Muleba kutokana na ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya maji. 
“Suala mojawapo ambalo bado linahitajika kutupiwa jicho la karibu ndani ya mkoa huu ni suala la maji, na hii ni kwa sababu mkoa huu una upungufu wa vyanzo vya uhakika vya maji hasa wilayani hapa Muleba,” amesema Samia.
 Amefafanua kuwa wananchi wengi wa Muleba wamekuwa wakitegemea mito na visima visivyo na uhakika, hasa wakati wa kiangazi na vipindi vya ukame, jambo linalosababisha usumbufu mkubwa kwa shughuli za kila siku. 
“Ninafurahi kuwapa taarifa kwamba tumefanya usanifu wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria… Tayari tumekamilisha upembuzi yakinifu kuyatoa maji kutoka Ziwa Victoria na kufanya maji haya safi na salama yatumike na Wanamuleba,” ameeleza. 
Dk. Samia amebainisha kuwa Wizara ya Maji ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa, na kuahidi kuwa serikali ya CCM itaendelea kutatua changamoto hiyo kwa wananchi wa Muleba na wilaya jirani zinazokabiliwa na upungufu wa maji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here