Nairobi, Kenya
Kamati ya Kitaifa inayoandaa Mazishi ya Kitaifa ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, imetangaza kwamba mazishi yake yatafanyika Jumapili nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, magharibi mwa Kenya.

Naibu Rais Kithure Kindiki, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo pamoja na kakake mkubwa wa Bw. Odinga Dkt Oburu Oginga, ametoa tangazo hilo katika hotuba ya kitaifa muda mfupi uliopita.
Kulingana na familia hiyo, Odinga aliomba kuzikwa ndani ya muda mfupi iwezekanavyo, ndani ya saa 72. “Tumeamua kuharakisha mchakato wa maandalizi ya mazishi ya Odinga kwa kusawazisha matakwa ya Odinga, matakwa ya familia, jamii, na masharti mengine ambayo lazima izingatiwe,” imeeleza kamati hiyo.
Mwili wa Raila Amolo Odinga unatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi kutoka India. Kutoka uwanjani JKIA, mwili utapelekwa moja kwa moja katika makafani ya Lee na baadaye kupelekwa katika Bunge la kitaifa ambapo Wakenya watapata furda ya kutoa heshima zao za mwisho kuanzia saa sita mchana.
Baadaye, mwili utarudishwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee Funeral Home kwa maandalizi ya mwisho. Ijumaa, ibada ya kitaifa ya mazishi itafanyika katika Uwanja wa Nyayo.
Viongozi kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo, ambayo itasimamiwa kama ibada rasmi ya kitaifa. Jioni ya siku hiyo, mwili utafikishwa nyumbani kwake Karen ambapo utalazwa kwa mara ya mwisho.
Jumamosi, mwili utasafirishwa hadi Uwanja wa Moi, Kisumu, ambapo wananchi wataruhusiwa kuuaga kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri.
Kutoka hapo, msafara wa mazishi utaelekea kwa barabara hadi Siaya. Maziko yatafanyika Jumapili nyumbani kwake Bondo.