Home KITAIFA Kima cha chini mishahara sekta binafsi chaongezeka-Ridhiwani

Kima cha chini mishahara sekta binafsi chaongezeka-Ridhiwani

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

SERIKALI imetangaza nyongeza ya Kima cha chini cha Mshahara kwa sekta binafsi ambapo kimepanda kwa asilimia 33.4 hatua inayolenga kuongeza tija na kukuza ari ya wafanyakazi wa kuongeza tija na uzalishaji.

Akitangaza nyongeza hiyo , leo Oktoba 17, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete amesema mchakato wa upangaji wa kima kipya cha chini cha mshahara umekamilika na kwamba umezingatia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 39 (1) cha Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura 300.

“Kwa mujibu wa Amri hiyo, Sekta za Kima cha chini cha Mshahara zimeongezeka kutoka 13 za mwaka 2022 hadi 16 kwa mwaka 2025 na kutoka sekta ndogo 25 za mwaka 2022 hadi 46 kwa mwaka 2025. Aidha, Kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 33.4 kutoka Shilingi 275,060/= hadi 358,322/= na kitaanza kutumika rasmi tarehe 1 January, 2026,”amsema Kikwete.

Kwa mujibu wa Ridhiwani , Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara imegusa sekta za kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi na huduma ya baharini, michezo na utamaduni pamoja na huduma nyinginezo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara kwa Sekta Binafsi, Dk. Suleiman Rashid Mohamed alisema mchakato wa majadiliano ulikuwa shirikishi ambapo vyama vya wafanyakazi, waajili na waajiliwa vilishiriki kikamilifu katika hatua zote.

Naye Naibu Katibu Mkuu Shirikishio la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Rehema Ludanga alisema kitendo cha Serikali kutangaza amri ya kupanda kwa mishahara kwa kima cha chini cha sekta binafsi ni faraja kwa wafanyakazi nchini kwani kimeonesha dhahili namna Serikali inavyothamini maslahi ya wafanyakazi nchini.

Ameongeza kuwa ni wakati sasa waajili wote katika sekta binafsi kutekeleza amri hiyo kwa kupandisha mishahara ikibidi zaidi ya kiwango kilichotangazwa ili kuongeza maslahi bora ya wafanyakazi wao .

Naye Afisa Mtendaji Mkuu Chama cha Waajili Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba – Doran ameeleza kuwa Chama kilishiriki kikamilifu kwenye mchakato kupitia kamati ya wataalam ambapo maoni yote yaliyokusanywa toka mikoa yote nchini na yamefanyiwa kazi hatua inayotoa urahisi wa utekelezaji wa amri hiyo.

Pia aliwasihi waajili kutumia muda huu kabla ya kufika tarehe 01 Januari 2026 kufanya mazungumzo yatakayopelekea kubadilisha ulipaji wa mishahara kwa mujibu wa amri iliyotangazwa na Serikali na kwamba ATE itaendelea kutoa elimu na taarifa kwa waajili wote nchini kutekeleza amri hii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here