Home KITAIFA DCEA yakamata kilo 10,783 za dawa za kulevya

DCEA yakamata kilo 10,783 za dawa za kulevya

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kati ya mwezi Septemba na Oktoba 2025, imekamata jumla ya kilogramu 10,783.94 za aina mbalimbali za dawa za kulevya, pamoja na kilogramu 6,007 na lita 153 za kemikali bashirifu katika operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali nchini huku jumla ya watuhumiwa 89 walikamatwa kuhusiana na uhalifu huo.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 21 2025 jijini Dar es Salaam na Kamisha wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, zilikamatwa dawa ya kulevya aina ya mirungi iliyokaushwa na kufungwa kama viungo (spices) yenye uzito wa kilogramu 40.32. Dawa hizo zilikuwa kwenye paketi 80 zenye maandishi “dry basil leaves”, na zilikuwa tayari kusafirishwa kwenda Canada na Italia.

“Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Yusuphu S. Kibaha (35) na Mohamed H. Ramadhan (41). Taarifa za kiuchunguzi zimebainisha kwamba, dawa hizo za kulevya ziliingizwa nchini kwa njia ya kificho kutokea nchi jirani na zilitumwa kupitia makampuni ya usafirishaji,” amesema.

Katika operesheni nyingine iliyofanyika eneo la Mlalakuwa, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Bright A. Malisa (26), Humphrey G. Safari (26), Novatus A. Kileo (26) na Chriss P. Mandoza (26) walikamatwa wakitengeneza biskuti za bangi 140 puli nane, na paketi tisa za bangi zenye jumla ya kilogramu 2.858.

Aidha, katika operesheni zilizofanyika katika mikoa ya Morogoro, Simiyu, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Tanga, Pwani, Shinyanga, Ruvuma, Tabora na Mtwara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, Lyimo amesema zilikamatwa bangi kilogramu 9,164.92, mirungi kilogramu 1,555.46, skanka gramu 367 na heroin gramu 7.498 na kuteketeza ekari 11.5 za mashamba ya bangi.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imesema inaendelea kujizatiti na kuhakikisha Tanzania inabaki salama na huru bila biashara na matumizi ya dawa za kulevya na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mtu atakayebainika kujihusisha kwa namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here