Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Samia Suluhu Hassan amesema ndani ya Miaka mitano ijayo ikiwa Chama chake kitapewa ridhaa ya kuunda serikali, watajenga daraja la Jangwani litakalokuwa na urefu wa Mita 390 pamoja na soko kubwa la kisasa katika eneo hilo kwaajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo.

Amesema kufikia sasa tayati taratibu zote za kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo zimekamilika isipokuwa jambo moja pekee wanalolisubiri, akisema daraja hilo mbali ya kupendezesha Jiji la Dar es Salaam, litarahisisha pia shughuli za usafiri na usafirishaji na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na Kijamii.
Ametoa ahadi hizo Jumatano Oktoba 22, 2025 Dk.Samia wakati wa Mkutano wa Kampeni za uchaguzi Mkuu wa Tanzania kwenye Viwanja vya Kecha, Kinyerezi, Wilayani Ilala Mkoani Dar es Salaam, akiahidi pia ujenzi wa madaraja mengine Mkoani humo likiwemo daraja la Mzinga Wilayani Ilala.
“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2025/30 imemuelekeza kujenga barabara za juu (Flyover) katika Makutano ya barabara Tabata, Buguruni na Fire ili kuondoa msongamano wa magari kwenye Jiji hilo lililo kitovu cha biashara Tanzania,”amesema.

Aidha Dk. Samia amesema ikiwa Watanzania watampa ridhaa ya kuunda serikali, miongoni mwa mambo atakayoyafanya mapema ni pamoja na kupokea ripoti za Tume aliyoiunda ya Marekebisho ya mifumo ya kodi nchini na Tume mbili ya tathmini kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa eneo la Hifadhi la Ngorongoro Mkoani Arusha.
Amesema tume nyingine ambayo itakabidhi ripoti yake kwa Dk. Samia ni Tume ya tathmini ya utekelezaji wa uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha, amesema atachukua hatua stahiki kulingana na maoni ya wananchi na mapendekezo waliyoyaeleza kwa Tume hizo zilizochukua maoni yao.

“Tume hizi zilishindwa kukabidhi ripoti zao licha ya kumaliza kazi yake kutokana na mwingiliano wa ratiba za Kampeni na Uchaguzi Mkuu wa Tanzania,”amesema.
Ameeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye mabadiliko na mageuzi mbalimbali anayoyachukua ikiwemo kurejea kwa heshima ya Tanzania Kimataifa pamoja na kuimarisha mahusiano yake ya Kidiplomasia, suala ambalo limekuza heshima ya Tanzania Kimataifa.
Akizungimzia kuhusu Dk.Samia Malengo ya Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi ilikuwa ni pamoja na kuchambua sera na sheria za kodi na kubaini maeneo ya kuboresha, kubaini athari za viwango vya kodi katika sekta ya uchumi, kufanya mapitio ya mifumo na mbinu za ukusanyaji wa mapato ya kodi na ya siyo ya kodi pamoja na kuchambua usimamizi na utekelezaji wa sheria za kodi na kuchambua mapato ya siyo ya kodi na namna yanavyoathiri sekta za uzalishaji.

Mengine ni kubainisha changamoto zinazoathiri utendaji wa mamlaka zinazosimamia ukusanyaji wa kodi, ushuru, tozo na ada mbalimbali, kuchambua usimamizi wa mapato ya mamlaka za udhibiti na serikali za mitaa, kupokea na ku chambua maoni na mapendekezo ya wananchi na wadau, kupata uzoefu kutoka kwenye nchi ningine kuhusu masuala ya kodi na kuandaa ripoti na mapendekezo jumuishi.