Home KITAIFA UDSM yaboresha tehama kupitia mradi wa heet

UDSM yaboresha tehama kupitia mradi wa heet

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu yake ya TEHAMA kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET), hatua itakayoongeza kuimarisha ufanisi katika ufundishaji, ujifunzaji na utoaji wa huduma za kimtandao chuoni .

Uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA ni hatua muhimu sana katika nyakati za sasa ambapo elimu na kazi nyingi za utawala zinategemea teknolojia ya kisasa. Hiyo itawawezesha wanafunzi, wahadhiri, na wafanyakazi kupata huduma bora na urahisi wa kufanya kazi kwa njia ya kidijitali.

Akizungumza Oktoba, 21 jijini Dar es Salaam na Wahariri wa Vyombo vya Habari mbalimbali waliotembelea utekelezaji wa mradi, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, amesema UDSM sasa ina uwezo wa kupokea na kusambaza mtandao wa 10Mbps kutoka uwezo wa awali wa 1.5Mbps, jambo litakalorahisisha upatikanaji wa taarifa na maudhui ya masomo kwa njia ya kidijitali.

Amesema chuo kinaendelea kuziunganisha kampasi zake zote kwa mtandao wa ndani ili kuwezesha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na kujisomea, sambamba na ujenzi na ufungaji wa vifaa vya kisasa vitakavyowezesha maandalizi na uendeshaji wa masomo pamoja na mitihani kwa njia ya mtandao.

“Mradi huu umewezesha uundaji wa mifumo ya kisasa ya masomo ambayo inatambulika kimataifa na inaweza kutumiwa pia na wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hadi sasa, masomo 1,000 yamekwishaingizwa katika mfumo huu,”amesema.

Ameeleza kuwa kuna kumbi za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 8,000 kwa wakati mmoja zimewekewa vifaa vya kisasa vya kufundishia, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya mazingira ya kusomea.

“Kwa sasa wanafunzi 39,000 wakiwemo 165 wenye mahitaji maalum pamoja na walimu 600 wameshaingizwa kwenye mfumo huu,” amesema.

Aidha amesema kupitia Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (CVL), jumla ya wahadhiri 377 wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya mifumo hiyo, na mafunzo kwa wahadhiri wengine yanaendelea. Utekelezaji huo, amesema, unaiweka UDSM katika nafasi ya kuwa kinara wa mageuzi ya kidijitali katika elimu ya juu nchini.

Kuhusu maboresho ya taaluma, Profesa Anangisye amesema jumla ya mitaala 250 imefanyiwa mapitio ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na uchumi wa kisasa.

“Mitaala hii imeandaliwa kwa kuzingatia ushauri wa wadau, hususan waajiri. Tumeongeza msisitizo kwenye mafunzo kwa vitendo ili mhitimu wa UDSM awe na maarifa, ujuzi na amali kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amepongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, akisema majengo yanayojengwa yanaonyesha kiwango kikubwa cha utaalamu na ubunifu.

“Leo tumeshuhudia majengo makubwa na mazuri yanayojengwa hapa UDSM kupitia mradi wa HEET. Nawapongeza kwa uhandisi mzuri na usimamizi bora. Vyombo vya habari tutaendeleza ajenda ya ubunifu wa chuo hiki na kuujulisha umma,” amesema Balile.

Pia amewataka Watanzania kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani wakati wa uchaguzi ujao kwa kusema, “Wiki ijayo tunapiga kura, chagueni viongozi mnaowataka, kura yako ndiyo itakayohesabika siyo vurugu.”

Profesa Anangisye alihitimisha kwa kusema kuwa Mradi wa HEET ni ukurasa mpya katika historia ya elimu ya juu nchini Tanzania, na kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaendelea kuzalisha wahitimu wabunifu, waadilifu, na wenye uwezo wa kuongoza nchi kuelekea uchumi wa kati na wa ngazi ya juu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here