Home KITAIFA Wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba,29

Wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba,29

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

MUUNGANIKO wa Asasi za Kiraia  Wanawake  na Watetezi wa Usawa wa kijinsia  hususan wanawake na vijana umeto wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki  katika zoezi la kupiga kura utakaofanyika Oktoba, 29 mwaka huu.

Pia wameikumbusha jamii kuwa katika kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi, ni muhimu jamii kuepuka lugha za kejeli, udhalilishaji na mashambulizi ya kibinafsi hasa kwa misingi ya kijinsia badala yake, mjadala wa kisiasa ujikite katika sera, ilani, na hoja zenye kujenga taifa.

Wito huo umetolewa leo Oktoba,  23 jijini Dar es Salaam wakati akisoma tamko la Asasi za Wanawake kuelekea uchaguzi Mkuu Mmoja wa Waanzilishi wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) na Mwandishi Mkongwe, Rose  Mwalimu,  amesema Tanzania haijashindwa  kumpata Rais mwanamke bali imepiga hatua kubwa kupitia yeye katika kutekeleza Dira ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5) inayosisitiza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika maamuzi.

Amesema kupitia Rais huyu mwanamke tumeona sheria kadhaa zikibadilishwa ikiwamo ya vyama vya siasa na hata miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya afya. 

“Ushiriki wa wanawake katika siasa unaongeza uwajibikaji, uwazi, na ustawi wa kijamii, kwa kuwa tafiti nyingi zinaonesha kwamba wanawake viongozi wanapendelea sera zinazogusa elimu, afya, haki za watoto, na usawa wa kiuchumi,” amesema.

Ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania imepata kiongozi mkuu wa nchi mwanamke, Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, ambaye pia anawania kiti hicho cha urais kwa tiketi ya CCM. Kadhalika, mwaka huu kumekuwa na wagombea wengine wanawake wa urais, akiwemo Saumu Rashid kutoka UDP na Mwajuma Mirambo UMD.

“Kwa upande wa wagombea wenza wa urais kutoka vyama vingine ni pamoja na Eveline Wilbard Munis (NCCR), Husna Mohamed Abdallah (CUF), Aziza Haji Selemani (D. MAKINI), Amani Selemani Mzee (TLP), Chausiku Khatibu Mohamed (NLD), Sakia Mussa Debwa (SAU), Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja (CHAUMA).

“Hii ni hatua kubwa ya kidemokrasia kwa Tanzania na kwa ajenda ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi,”amesema.

Amesema uongozi wa mwanamke si tishio bali ni nyenzo ya kuimarisha demokrasia jumuishi, yenye kusikiliza na kutenda kwa manufaa ya wote.

Aidha ameikumbusha  Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa, na wadau wote kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanakuwa salama, jumuishi, na huru dhidi ya vitisho, udhalilishaji, na ukatili wa kijinsia, ambao mara nyingi huwakatisha tamaa wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa.

“Hivi karibuni, tumemsikia Rais wa Tanzania ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan, akisema katika mkutano wa kampeni jijini Dar es Salaam:

Niwaombe ndugu zangu, twendeni mkapige kura… Ndugu zangu mengine niachieni mimi, matusi niachieni mimi, ninayabeba kwa niaba yenu. Niliapa kuwa Rais wa Tanzania, niliapa kuilinda nchi hii kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano wetu.

“Kwa kauli hiyo, tunapenda kuuambia umma kuwa uongozi wa mwanamke si tishio bali ni nyenzo ya kuimarisha demokrasia jumuishi, hivyo tunawakumbusha Watanzania kuwa mwanamke kiongozi anaposhika madaraka asihukumiwe kwa jinsia yake, bali kwa uwezo, uzoefu na dira yake ya maendeleo,”alisema Mwalimu.

Ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake kuratibu midahalo, makala, na mijadala inayojenga uelewa wa umma juu ya uwezo na mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Lucy Kilasi kutoka Asasi ya  Welfare Tanzania, amesisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa wanawake katika kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia.

Amesema kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ni moja ya vipaumbele vya mashirika ya kijamii kwani uwepo wa wanawake viongozi utachochea maendeleo nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here