Na Mwandishi wetu, Mpanda
HALMASHAURI ya Manispaa ya Mpanda na Mkandarasi M/s Chonqing International Construction Corporation (CICO), wametiliana saini mkataba wa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa Kilomita 8.4.

Makubaliano hayo ya mradi huo wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC), yanajumuisha ujenzi wa barabara 10 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa jengo la usimamizi wa mradi na magari manne ya kusimamia utekelezaji wa mradi.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Oktoba 25, 2025 katika halfa iliyofanyika mjini Mpanda mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC, Mhandisi Emmanuel Manyanga, amesema mradi huo utatekelezwa kwa miezi 15 kuanzia Novemba Mosi, 2025.
“Ujenzi wa miundombinu hii utahusisha barabara za Mkumbo Junction – Nsemulwa Health Center (Km 1.68), Nsemulwa Health Center – Sokoine (Km 1.23) Kapufi (Mita 760, Sumry (Mita 460), Pinda (Mita 260) Fimbo ya Mnyonge (Mita 390) Fish Market (Mita 330), Mpanda Hotel (Mita 760), Mikocheni Junction – White Gireffe (Km 1.88) na Homeground (Mita 730),” amesema Manyanga.

Mhandisi Manyanga amesema mradi huo utasimamiwa na Mshauri Elekezi M/s NIB Plan Consult Limited kutoka Dar es Salaam.
Aidha, ameeleza kuwa mradio wa TACTIC utagharamia pia kuandaa mipango kabambe (Master Plans) kwa miji 19 iliyo chini ya Mradi huo.
“Pamoja na uboreshaji wa miundombinu, pia mradi huu una kipengele cha kujengea uwezo taasisi zote za Wizara, TARURA pamoja na Halmashauri za Miji kupitia mafunzo mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji kazi, ufanisi wa huduma mbalimbali kwa jamii pamoja na kununua vitendea kazi kama vile magari ya usimamizi na ufuatiliaji, pamoja na kuhuisha mifumo ya ukusanyaji mapato,” amesisitiza Mhandisi Manyanga.

Kwa upande mwingine wananchi wa Mkoa huo, wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao utaboresha mandhari ya mji huo na kukuza uchumi wa wananchi wake.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa huo, Vicent Longino Nkana, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa inayoendelea kufanya hasa ya kuboresha miji ambayo hapo awali ilikuwa mapori na mingine haina mvuto.
“Dk. Samia amefanya kazi nzuri sana ya kutuletea wananchi maendeleo kama mradi huu kwenye mji wetu, ametufaa sana na tunamshukuru kwa kazi kubwa anayoendelea kufanya, “ amesema Nkana.

Aidha, ameiomba TARURA kuwajengea barabara nyingine za mji huo ili kuendelea kuunganisha na kukuza uchumi wa wananchi hao.
Mradi wa TACTIC ni mojawapo ya miradi inayofadhiliwa na Serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 410 (Bila VAT).
Malengo ya mradi huu ni kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania pamoja na kujengea uwezo taasisi (Halmashauri) ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendelezaji miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Lengo kuu la mradi wa TACTIC ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma bora kwa wananchi.



