Na Mwandishi wetu, Mara
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia hivi karibuni kuijengea uwezo hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mara kutoa matibabu ya kibingwa na kibobezi ya wagonjwa wa majeruhi wa ajali, mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Seif Shekalaghe ya kuzijengea uwezo hospitali za rufaa za mikoa ili kupunguza rufaa zinazoenda MOI na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Hayo yamebainishwa Okyoba 24, 2025 na Mkurugenzi wa huduma za upasuaji wa mifupa MOI Dk. Anthony Assey wakati wa ziara ya jopo la wataalamu kutoka MOI walipotembelea hospitali hiyo ili kukagua miundombinu iliyopo hospitalini hapo ikiwa ni maandalizi ya ujio wa madaktari bingwa na bobezi toka MOI kuja kutoa huduma hospilini hapo.

‘’Ujio wetu ni utekelezaji wa maagizo ya Dkt. Shekalaghe ya kuzijengea uwezo hospitali za rufaa za mikoa kutoa huduma za kibingwa na bobezi za matibabu ya majeruhi wa ajali, huduma za wagonjwa mahututi (ICU), mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu pia kusogeza huduma za MOI karibu na wananchi,” amesema Dk. Assey.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya amesema kuwa ujio wa wataalam kutoka MOI kutawapunguzia gharama wananchi wa mkoa wa Mara za kuzifuata huduma hizo MOI, Dar es Salaam na itazidi kuimarisha tiba utalii kwani wanahudumia wagonjwa wengi kutoka Kenya.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Zabroni Masatu amesema wanategemea hospitali hiyo kuwa kubwa zaidi kupitia kujengewa uwezo na MOI na wanaiomba Menejimenti ya MOI huko mbeleni kuanzisha tawi la MOI katika mkoa wa Mara.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi, Dk. Elias Godfrey amesema walikuwa wanausubiri kwa hamu ujio huo na wapo tayari kushirikiana na MOI ili kuzidi kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.



