📌 Jumla ya wateja 1,700 wamebainika kutumia umeme kinyume na taratibu.
📌 Yatoa onyo kali kwa wateja wanaofanya udanganyifu kurejesha umeme kwa kutumia vishoka baada ya kusitishiwa huduma
Na Agnes Njaala, Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikiwa kuokoa upotevu wa mapato unaokadiriwa kufikia shilingi bilioni 1.7, kufuatia utekelezaji wa zoezi la ukaguzi wa miundombinu ya umeme linaloendelea kote nchini.

Akitoa tathmini ya utekelezaji wa zoezi hilo mapema wiki hii , Meneja Msimamizi wa mfumo wa Mita, Mhandisi Nyanda Mlagwa, alisema ukaguzi huo ulianza mwezi Julai 2025 ukilenga kubaini matumizi yasiyo halali ya umeme na kudhibiti vitendo vya wizi unaosababisha hasara kwa Shirika na Serikali.
“ Napenda kuutarifu umma kuwa hadi sasa, ukaguzi uliofanyika umebaini upotevu wa takribani shilingi bilioni 4, ambapo zaidi ya bilioni 1 zimeshalipwa na wateja waliobainika kuwa na makosa, huku wengine wakiendelea kulipa madeni yao,” amebainisha Mhandisi Mlagwa.
Ameongeza kuwa mapato yanayopatikana yataelekezwa katika kuboresha huduma kwa wateja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme nchini.
Aidha, amesema baadhi ya makosa yaliyobainika ni pamoja na uunganishaji wa umeme kinyume na taratibu, uchepushaji wa nyaya kabla ya mita (bypass), uhamishaji holela wa mita, na kuchezea kufuli za mita (seal).

Ametoa wito kwa watanzania kutoa taarifa za wahujumu kupitia mfumo wa TANESCO wa Whistleblower ambao umekuwa ukisisitizwa kuwa ni mfumo bora na salama ili kusaidia kudhibiti vitendo vya uhujumu.
Mhandisi Msimamizi Kitengo cha Uthibiti wa Mapato Makao Makuu , Mposheleye Mwasenga alisema jumla ya wateja 1,700 katika kipindi tajwa wamebainika kutumia umeme kinyume na taratibu akisisitiza kuwa makadirio yote yamefanywa kwa usahihi kulingana na matumizi halisi na wote wameandikiwa madeni na faini kwa mujibu wa sheria na miongozo ya EWURA.
Ametoa onyo kwa wateja wanaofanya udanganyifu wa kurejesha umeme kwa kutumia vishoka, Mhandisi wa Uthibiti wa Mapato wa Mkoa wa Kinondoni Kusini, Salumu Mbepei, amesema kuwa Shirika lipo macho na limeunda timu maalumu ya kufuatilia vitendo hivyo, na kwamba wote watakaobainika watachukuliwa hatua kali zaidi za kisheria.

Naye Fundi Mkaguzi, Damasi Kimaro,ametaja mojawapo ya changamoto kubwa wanazokutana nazo wakati wa ukaguzi kuwa ni baadhi ya wateja kukaidi kuruhusu ukaguzi, hali inayokwamisha utekelezaji wa operesheni kwa ufanisi. Ameitoa wito kwa wateja kutoa ushirikiano kwa wakaguzi, akisisitiza kuwa zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Shirika linaendelea kuufahamisha umma kuwa utekelezaji wa mkakati wa kudhibiti upotevu wa mapato nchini ni endelevu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha matumizi sahihi ya huduma ya umeme na kuimarisha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.



