Na Mwandishi wetu, Geita
MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amewataka viongozi wa serikali za mtaa kushirikiana na halmashauri kufuatilia kwa ukaribu na kudhibiti uvamizi wa maeneo ya taasisi ikiwemo shule.

Kauli hiyo inakuja kufuatia kuripotiwa kwa changamoto ya baadhi ya wananchi kuvamia na kujenga ndani ya eneo la shule ya msingi Nyantindili iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Geita.
Shigela ametoa maagizo hayo akiwa katika ziara maalum ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Geita ikiwemo miradi ya elimu na barabara.
Amesema maeneo ya taasisi za umma ikiwemo shule yanapaswa kulindwa ili ziendelee kuwa na hifadhi ya aridhi ya akiba maalum kwa uendelezaji na upanuzi wa huduma pale inapohitajika.
Shigela ameongeza kuwa hifadhi ya maeneo ya taasisi unasaidia kuondoa ulazima wa serikali kulipa fidia kwa wananchi pale ambapo kuna mahitaji ya upanuzi wa huduma za kijamii.
“Haya maeneo siyo ya mkurugenzi, kwa hiyo tukiendelea kuruhusu maeneo yetu kuvamiwa, Watoto wetu watalazimika kutembea umbali mrefu kufuata shule zenye maeneo.
“Kwa hiyo ulinzi wa eneo hili usiwe wa Mwalimu Mkuu pekee yake, au mwenyekiti wa mtaa sisi sote tuulize tukiona mtu anajenga kwenye eneo la shule” amesema Shigela.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo amesema ulinzi wa raslimali za umma unashirikisha jamii nzima na kila mtu anawajibika.
Kamanda Jongo amesema katika kuunga mkono juhudi za serikali jamii nzima inapaswa kuisaidia serikali kwa kusimamia suala la malezi na kuwasimamia kikamirifu kuepuka tabia hatarishi.
Awali Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi, Nyantindili halmashauri ya manispaa Geita, Helen Ndimubenya amesema serikali imetoa sh milioni 163 kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
Helen amesema kati yake pesa za mradi wa Boost ni sh milioni 88.6, mapato ya ndani kiasi cha sh milioni 50 pamoja na pesa za serikali kuu kiasi cha shilingi milioni 25.



