*Watanzania Wote Watasikilizwa na Kuhudumiwa kwa Heshima
*Ajira na Kupambana na Umaskini
*Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050: Ajira Milioni Nane kwa Vijana
Na Esther Mnyika, Dodoma
WAZIRI Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba ameahidi kuwa serikali itahakikisha kila Mtanzania hususan wale wa ngazi za nchini wanasikilizwa na kuheshimiwa kila ofisi ya umma.

Akizungumza leo Novemba,13 2025 Bunge jijini Dodoma baada ya kuthibitishwa na Bunge Dk. Nchemba amesema serikali inazingatia uwajibikaji wa watumishi wa umma kwa wananchi na kujenga utamaduni wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja.
“Ninatambua uzito wa majukumu haya ya Uwaziri Mkuu pamoja na matarajio yake, pamoja na matarajio ya Watanzania. Nitafanya kazi kwa bidii, kwa uaminifu na jitihada kubwa kuweza kukidhi matarajio hayo,” amesema Dk. Nchemba.
Amesema anatambua mahitaji ya watanzania atasimamia kwa uadilifu na jitihada kuhakikisha hayo yanatimia hivyo watumishi wa umma na watanzania wote kuwa tayari kuenda kwa gia ya kupanda mlima.
“Nawaonya Watumishi wa umma ambao ni wazembe, wavivu na wala rushwa kujiandaa kukumbana na hatua kali mara baada ya kuanza kazi rasmi na serikali haitavumilia urasimu,uzembe wala lugha za matusi zisizofaa kwa wananchi, ” amesisitiza.
Amesema wananchi watasikilizwa muda wote kwa heshima kwenye ofisi zote za umma lazima wawe waadilifu na wenye kuwahudumia wananchi kwa wakati kama anavyotaka Rais Dk.Samia.
Ameongeza kuwa anataka kuona mabadiliko katika utendaji wa watumishi wa umma hasa katika utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuhakikisha serikali inatekeleza kwa vitendo dhamira ya kuwahudumia Watanzania wote kwa haki na ufanisi.
“Natambua matatizo ya ajira ya kwa vijana natambua maumaumivu ya kukosa ajira hivyo naahidi kushirikiana kwa karibu na Rais Dk.Samia kuhakikisha ajira zinapatikana na umaskini unaokadiriwa kufikia asilimia 26 na unaupungua kwa kiwango kikubwa nchini,” amesema Dk. Nchemba.
Akizungumzia kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 amasema Dira hiyo imeweka kipaumbele kwenye masuala ya ajira ikiwa lengo ni kutoa ajira milioni nane kwa vijana nchini.
Amesema Serikali awamu ya sita inayoingia katika awamu yake ya pili kusimamia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 ambayo inalenga kuleta mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii nchini.
Aidha amesema ameishi kwenye maisha ya umaskini kwa miaka 32, hivyo amewahakikishia Watanzania, hasa wenye maisha ya chini, kuwa watasikilizwa kwa nidhamu kwenye kila ofisi ya umma.
Dk. Nchemba amesema maisha aliyowahi kupitia tangu akiwa nyumbani kwa baba yake yamekuwa ya msingi wa dhamira yake ya kupambana na umasikini.
Amesimulia jinsi alivyokulia katika mazingira magumu na hata baada ya kuanza maisha ya ndoa na mkewe Neema waliendelea kukabiliana na changamoto za uchumi.
“Spika, mimi umasikini nimeuishi nyumba kwetu tuliishi maisha ambayo shuka ya kujifunika ilikuwa ni kanga anayojifunga mama au dada yako na kama muvua ikinyesha basi ngozi ndiyo unajifunika ili usilowane,”ameeleza Dk. Nchemba.



